Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe, wenzake waomba kesi yao kusubiri rufaa

11786 MBOWE+PIC TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi tisa wa Chadema akiwamo mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wamewasilisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu maombi ya kuomba kesi yao ya jinai namba 112/2018 kuahirishwa hadi rufaa yao itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo jana mbele ya hakimu Wilbard Mashauri na mawakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya na Peter Kibatala.

Wakili wa Serikali, Dk Zainabu Mango aliieleza mahakama kuwa wamepewa hati ya maombi hayo namba 10/2018 na wapo tayari kuwasilisha majibu kinzani kesho na kuwapatia upande wa utetezi.

Hata hivyo, Mtobesya aliomba wapewe siku mbili ili waweze kufaili majibu ya nyongeza kama watakuwa nayo. Baada ya kusikiliza pande zote, Mashauri aliamuru upande wa mashtaka kuwasilisha majibu kinzani Agosti 14 na iwapo upande wa utetezi utakuwa na majibu ya nyongeza utayawasilisha Agosti 16.

Alisema maombi hayo yatasikilizwa Agosti 21 na kesi ya msingi pia itatajwa siku hiyo.

Wakati hayo yakiendelea washtakiwa wote walikuwapo mahakamani. Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar). Wengine ni mbunge wa Tarime vijijini, John Heche; Halima Mdee (Kawe); Ester Bulaya (Bunda); Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); Esther Matiko (Tarime Mjini) na katibu mkuu wao, Dk Vincent Mashinji.

Chanzo: mwananchi.co.tz