Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe, wenzake wahitimisha harakati za kujinasua hatiani

98332 Mbowe+pic Mbowe, wenzake wahitimisha harakati za kujinasua hatiani

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi wakuu na wabunge wa Chadema wamefunga kazi baada ya kuwasilisha hoja zao za majumuisho, katika kesi ya jinai inayowakabili.

Viongozi hao, ambao ni pamoja na mwenyekiti Freeman Mbowe na katibu mkuu, John Mnyika wanakabiliwa na mashtaka ya 13 yakiwemo ya kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kusababisha woga na hofu kwa wakazi wa Kinondoni na kifo cha Akwelina Akwilini.

Jana, kiongozi wa jopo la mawakili wa viongozi hao wa Chadema, Peter Kibatala alilieleza Mwananchi jana kuwa tayari wamewasilisha hoja za majumuisho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu juzi na kwamba sasa wameiachia mahakama ifanye kazi yake.

Huo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa Februari 24 na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba aliyetaka pande zote katika kesi hiyo, kuwasilisha hoja zao za mwisho, baada ya washtakiwa kumaliza utetezi wao.

Hakimu Simba aliamuru wawasilishe kwa njia ya maandishi badala ya mdomo, kabla au Machi 3, kisha akapanga kutoa hukumu Machi 10.

Lakini wakili Kibatala alilieleza Mwananchi kuwa waliwasilisha hoja hizo siku moja baada ya tarehe waliyoagizwa kwa kuwa walichelewa kupata mwenendo wa kesi kutoka mahakamani kwa ajili ya kuandaa hoja hizo.

Pia Soma

Advertisement
Kuwasilishwa kwa hoja hizo kunahitimisha mapambano ya viongozi hao wa Chadema dhidi ya waendesha mashtaka wa Serikali katika kesi hiyo iliyodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Wakili Kibatala hakutaka kuweka wazi undani wa hoja zao, lakini kwa kawaida hoja za mwisho huwa ni uchambuzi wa ushahidi, utetezi na vifungu vya sheria kuhusu mashtaka yanayowakabili washtakiwa.

Katika uchambuzi huo wa ushahidi, utetezi na vifungu vya sheria hulenga kuionyesha mahakama jinsi upande wa mashtaka ulivyoweza au kushindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka kiasi cha kuwatia hatiani washtakiwa.

Hivyo mawakili wa utetezi katika hoja zao watakuwa wameonyesha ushahidi wa upande wa mashtaka kuishawishi mahakama kuwa umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa na hivyo hawana hatia kwa mashtaka hayo.

Pamoja na uchambuzi wa ushahidi, utetezi na vifungu vya sheria, pia watakuwa wameirejesha mahakama katika hukumu za kesi mbalimbali zilizokwishaamriwa na mahakama.

Hata hivyo jopo la mawakili wa Serikali, linaloongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi nalo litakuwa limeionyesha mahakama jinsi walivyothibitisha mashtaka dhidi ya wasahtakiwa na hivyo kuwatia hatiani.

Katika hilo watakuwa wamechambua na kuonyesha uzito wa ushahidi wao na jinsi ulivyowagusa washtakiwa hao kila mmoja, huku nao wakiirejesha mahakama katika hukumu za kesi mbalimbali zilizokwishaamuriwa na mahakama mbalimbali nchini kwa mashtaka kama hayo.

Mahakama pia katika hukumu yake katika kuwatia au kuwaona kuwa washtakiwa hawana hatia, itakuwa na wajibu wa kupitia ushahidi na hoja za pande zote, sheria pamoja na kesi rejea hizo zitakazowasilishwa na pande zote na hata kesi nyingine nje ya hizo zitakazowasilishwa na mawakili hao.

Mbali na Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, Kilimanjaro na Mnyika, mbunge wa Kibamba, Dar es Salaam, wengine ni naibu katibu mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Wengine ni Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na mbunge wa Tarime Mjini, Halima Mdee (mbunge wa Kawe), Esther Bulaya (Bunda), John Heche (Tarime Vijijini) na Dk Vincent Mashinji ambaye alikuwa katibu mkuu wa Chadema kabla ya kurejea CCM hivi karibuni.

Mbali na kutuhumiwa kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria Februari 16, 2018 wakati wa uchaguzi mdogo Kinondoni, Mbowe ana mashtaka mengine matano peke yake, huku Msigwa na Mdee nao wakikabiliwa na shtaka moja zaidi kila mmoja.

Mashtaka hayo ya Mbowe peke yake ni ya kuhamasisha chuki kwa jamii (mashtaka mawili), uchochezi (kutokana na maneno aliyoyatamka siku ya kufunga kampeni na ushawishi wa kutenda kosa, akidaiwa kuwashawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la mkusanyiko usio halali.

Msigwa pekee anadaiwa kutenda kosa la kuwashawishi wakazi wa Kinondoni kutembea na silaha mbele ya umma.

Chanzo: mwananchi.co.tz