Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe, vigogo Chadema kusimama kizimbani Kisutu siku tano mfululizo

9804 Mahakamani+pic TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na vigogo wenzake wanane watasimama kizimbani kuanzia Juni 25 hadi 29 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusomewa maelezo ya awali na kuanza rasmi kuisikiliza kesi ya jinai inayowakabili.

Viongozi hao wanaokabiliwa na mashtaka 13 walipaswa kusomewa maelezo ya awali jana mbele ya hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri lakini ilishindikana kwa sababu Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa kwanza amefiwa na kaka yake.

Pia, Mahakama imemtaka mshtakiwa wa tano, Esther Matiko ambaye ni mbunge wa Tarime Mjini, kuhudhuria mahakamani licha ya kuwa ni mgonjwa na kwamba, asipofanya hivyo hatua dhidi yake zitachukuliwa.

Hata hivyo, mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya hawakuwapo jana mahakamani, Kibatala alikuwa anahudhuria kesi Mahakama Kuu huku Mtobesya akiwa anahudhuria kesi Mahakama ya Afrika Mashariki Arusha.

Hivyo, waliwakilishwa na mawakilI Nashon Nkungu, Frederick Kihwelo na Hekima Mwesigwa.

Awali, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi alieleza kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na kwamba walikuwa wamejipanga kuendelea.

Washtakiwa waliokuwepo mahakamani ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Chanzo: mwananchi.co.tz