Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbaroni wakidaiwa kuvamia maduka, wamo askari kampuni za ulinzi

Mbaroniiiiiiiii Mbaroni wakidaiwa kuvamia maduka, wamo askari kampuni za ulinzi

Thu, 25 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikilia watu 12 wakiwemo askari wa kampuni za ulinzi waliokuwa wakilinda maduka ya wafanyabiashara yaliyovamiwa na kuporwa fedha katika maeneo ya Katoro na Kamena wilayani Geita.

Mwishoni mwa Aprili mwaka huu, maduka ya bidhaa mbalimbali na vibanda 22 vinavyotoa huduma za kifedha katika eneo la Kamena na Njiapanda ya Kanyala kwenye mji mdogo wa Katoro yalivamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kufanikiwa kupora zaidi ya Sh17 milioni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema mbali na walinzi, watu wengine wanne wanashikiliwa baada ya kupata taarifa za siri kuwa wanahusika kwenye uhalifu huo.

Amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi hilo umebaini askari wa ulinzi kutoka kampuni binafsi za ulinzi wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu kwenye maduka nyakati za usiku.

“Tulichogundua maduka yaliyovamiwa yanalindwa na idadi kubwa ya walinzi na wanasilaha lakini hawazitumii na badala yake wanakimbia na hawatoi taarifa, uchunguzi unaonyesha walinzi hao wanatoa mwanya ili wezi waweze kufanya uhalifu,”amesema Jongo

Kamanda Jongo amesema katika kukabiliana na matukio hayo wameanza kutoa elimu ya ulinzi shirikishi kwa wananchi pamoja na kuhuisha vikundi vya ulinzi vikiwemo sungusungu ili kuhakikisha raia na mali zao wanakuwa salama.

Hata hivyo amezitaka kampuni za ulinzi kufanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kabla ya kuajiri kutokana na uchunguzi kubaini walinzi wengi ni wahalifu na wanapata kazi kwa kughushi vyeti kisha kushirikiana na majambazi kufanya uhalifu.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amesema Serikali ya wilayani humo kwa kushirikiana na jeshi la polisi wamejipanga kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa na wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Amewataka wananchi kutambua mlinzi namba moja wa mali ni mwananchi mwenyewe hivyo kuwataka wajilinde na kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wanatokomeza matukio hayo yaliyoanza kushamiri kwenye wilaya hiyo siku za hivi karibuni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live