Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbaroni wakidaiwa kutengeneza pombe feki

Pombe Kibali Mbaroni wakidaiwa kutengeneza pombe feki

Fri, 1 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewakamata watu sita akiwemo Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza vinywaji cha Dalton, kwa tuhuma za kuendesha kiwanda cha kutengeneza pombe bandia wakitumia chapa halisi za vinywaji vikali vilivyopo sokoni.

Akizungumza jana Agosti 31, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amethibitisha kushikiliwa kwa watuhumiwa hao na kwamba wapo katika mahabusu za jeshi hilo.

"Ni kweli hao watuhumiwa wapo kwetu lakini tunashindwa kuzungumzia kwa sababu sio watu wetu ni wa TRA, sisi tumekuja tu kuombwa mahabusu wakati taratibu zingine za kisheria zikiendelea," amesema Masejo

Watuhumiwa hao wamekamatwa Agosti 29 wilayani Longido, mkoani Arusha katika mpaka wa Namanga ndani ya Dalton Beverage Factory.

Ukamataji huo wa kushtukiza umefanika usiku ukiongozwa Mkuu wa Wilaya ya Longido Marko Ng’umbi aliyeongozana na maofisa wa TRA, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Uhamiaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ng'umbi amewataja wengine waliokamatwa kuwa ni pamoja na meneja wa kiwanda, Kelvin Philipo, wafanyakazi wengine Judith Mwande, Nduku Mutua na Lucy Kanini Mutua.

"Mwingine ni mtu mwenye sura ya kuogofya ambaye alionekana amepoteza akili na alipatikana akiwa amefungiwa ndani ya chumba kilichofanana na ngome, mate yakitoka. Utambulisho wake haujulikani hadi sasa," amesema.

Amesema kiwanda hicho kilikuwa kinaendeshwa na Wakenya na Watanzania ambao wamekuwa wakitengeneza na wakiweka pombe hizo kwenye chupa za vinywaji vilivyokuwa tayari zimetumika na kutupwa kama vile gin, bia whisky na konyagi zinazozalishwa katika nchi hizo mbili jirani.

Amesema kuwa wazalishaji hao walikuwa wananunua chupa za vinywaji hivyo kutoka kwa vijana mbali mbali mbali mtaani kisha kuosha kwenye matanki yao kabla ya kumiminia pombe walizotengeneza na kufungasha na kuleta muonekano kama kinywaji husika cha kifungashio hicho kisha kusambaza kwa ajili ya mauzo.

Aidha Kiwanda hicho pia kilikuwa na mashine ya uchapishaji ya kuzalisha bidhaa ghushi, lakini pia mihuri ya mapato yenye sura halisi na stempu kutoka TRA, Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA), na Mamlaka ya Mapato ya Malawi.

Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Edwin Changwe, amethibitisha mihuri hiyo kughushiwa na ukwepaji wa zaidi ya Sh100 milioni za tozo za ushuru.

"Mihuri hiyo ni ya kughushi lakini inaonekana kama halisi na kama shehena hiyo ingekuwa ya kweli, mtoza ushuru angepata zaidi Sh100 milioni, hivyo tunakwenda kujiridhisha na makosa haya ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake."

Ofisa wa TBS mpakani Namanga, Domisian Saasita, amesema wamechukua sampuli za vinywaji vinavyotengenezwa katika kiwanda hicho cha siri na kuvipeleka kwa Mkemia wa Serikali ili kufanyiwa uchunguzi iwapo vinafaa kwa matumizi ya binadamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live