Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbaroni madai kumuua mama mzazi kwa panga

Tanga.webp Mbaroni madai kumuua mama mzazi kwa panga

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

POLISI mkoani Tanga, inamshikilia Abdrahman Dihela (40), mkazi wa kijiji cha Kwachaga, Wilaya ya Handeni kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi kwa kumkata panga na kumtenganisha shingo na kiwiliwili kwa tuhuma za kishirikina.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Blasius Chatanda, alisema kuwa tukio hilo limetokea Mei 4, mwaka huu katika Kijiji cha Kwachaga, Wilaya ya Handeni.

Mtuhumiwa huyuo anadaiwa kumuua mama yake mzazi Asha Mwandenye (66).

Chatanda alieleza kwamba mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mama yake kuwa anamfanyia ushirikina na kusababisha maisha yake kuwa mabaya na kutoweza kuendelea kwa kila anachokifanya.

“Kitendo hiki ni cha kikatili sana na kwa akili za kawaida mtu huwezi kukifanya labda uwe na upungufu wa akili, tulichokifanya ni kumchukua mtuhumiwa na muda wowote kuanzia sasa atapelekwa mahakamani kusomewa shtaka lake,” alisema Chatanda.

Wakati huo huo, katika kijiji cha Moa wilayani Mkinga jeshi hilo limemkamata Mohamedi Mambo (43), mkazi wa Kisosora mjini Tanga, akiwa na dawa za kulevya aina ya mirungi.

Kamanda Chatanda alieleza kwamba mtuhumiwa alikuwa akisafirisha mirungi hiyo iliyokadiriwa kuwa na kilo 250, kwa kutumia boti ndogo aliyokuwa akiiendesha huku akiwa na wenzake wawili ambao walifanikiwa kutumbukia kwenye maji na kutoroka.

Alisema kuwa jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa pamoja na boti yake na ikithibitika kuwa yeye ndiye muhusika wa dawa hizo, boti hiyo pia itataifishwa na serikali.

Chatanda aliendelea kuwaasa wananchi mkoani hapa kufanya kazi za halali zitakazowaingizia kipato bila usumbufu wa Jeshi la Polisi kwa kuwa operesheni hiyo itakuwa endelevu ndani ya mkoa.

“Kama nilivyosema awali hili zoezi ni endelevu la kufanya operesheni zetu kila siku na kuwakamata wale wote wanaokwenda kinyume na matakwa ya serikali, wanaodhani biashara kama hizi zinafaa mimi nawakatalia na sasa watafute kazi au biashara nyingine za kufanya kwa kuwa biashara haramu itawaletea umaskini,” alisisitiza kamanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live