Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbaroni kwa tuhuma za kuiba kichanga kituo cha afya

Handcuffed Woman Tukio hilo lilitokea Februari mosi, mwaka huu

Mon, 21 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mkazi wa Kata ya Lugunga wilayani Mbogwe mkoani Geita, Rehema Saidi (47) kwa tuhuma ya kuiba mtoto mchanga wa siku 20 katika Kituo cha Afya Lunguya kilichoko Halmashauri ya Msalala mkoani hapa.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga (ACP) Joseph Haule, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo Februari 17, mwaka huu, akiwa na mtoto huyo baada ya kufanyika kwa upelelezi.

Alisema tukio hilo lilitokea Februari mosi, mwaka huu, majira ya saa 11 jioni kwenye Kituo cha Afya Lunguya.

Kamanda Haule alisema mtoto huyo ambaye ni wa kiume aliibiwa kitandani na kupatikana wilayani Mbogwe mkoani Geita akiwa mikononi mwa mtuhumiwa huyo.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Betha Augustino (21), alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi kwa kufanikisha kupatikana kwa mtoto wake.

“Ninafuraha kumpata mwanangu, naipongeza serikali hususani Jeshi la Polisi na vyombo vya habari kwa kuchapisha habari zilizosababisha mwanangu kupatikana kwani watu wengi wamenipigia simu baada ya kusoma taarifa hizo,”alisema Augustino.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Novelt Furaha aliomba serikali kuimarisha ulinzi katika vituo vya afya, zahanati na Hosptali ya Wilaya ili kudhibiti matukio ya wizi wa watoto hususani katika wodi za kujifungulia.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Msalala, Dk. Joseph Muyeye, alikili kutokea tukio la wizi katika kituo cha afya hicho na kwamba mtoto huyo amechunguzwa afya yake na kukutwa yupo vizuri.

Alisema aliyemuiba mtoto huyo alikuwa anamnywesha maziwa ya ng’ombe hivyo wamewashauri wazazi hao waendelee kumnywesha maziwa hayo bila kumbadilishia.

Alisema ili kuendelea kudhibiti vitendo vya aina hiyo wameweka madaftari maalum ya kusaini unapoingia na kutoka katika wodi zote zilizoko katika vituo vya afya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live