Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbaroni kwa kukwepa kodi ya Ardhi ya Bil. 4

RUNGU watu hao ni wadaiwa sugu wa halmashauri ya Nyamagana

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wadaiwa sugu 400 wa kodi ya ardhi wamefikishwa katika Mahakama ya Ardhi ya Mkoa wa Mwanza kwa kushindwa kulipa kodi ya ardhi ya zaidi ya Sh4.2 bilioni.

Kamishina wa ardhi Mkoa wa Mwanza, Eliah Kamiyanda amesema watu hao ni wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana na Ilemela.

Amesema kwa mujibu wa taratibu za kisheria zipo hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Idara ya Ardhi katika kuwaelimisha na kuwakumbusha wananchi wajibu wao kulipa kodi ya ardhi ingawa wengi wao hawafanyi hivyo.

“Kutokana na tatizo hilo, kupitia kifungu cha 50 cha Sheria ya Ardhi, mtu yeyote anayekaidi kulipia kodi ya ardhi, Kamishina ana wajibu wa kuwafikisha mbele ya sheria watu hao ili waweze kujibu mashtaka yao,” amesema Kamiyanda.

Amesema ofisi hiyo inakusanya kodi ya ardhi kwa mujibu wa sheria na kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, iliweza kukusanya zaidi ya Sh8 bilioni huku watu ambao walikaidi kulipa walifikishwa mahakamani.

“Kama ofisi ya ardhi mwaka huu, tumejiwekea malengo ya kukusanya zaidi ya Sh18 bilioni,” amesema Kamiyanda huku akituma ujumbe kwa walipa kodi katika wilaya zingine za Mkoa wa Mwanza kuhakikisha wanajitokeza kulipa kodi hizo ambapo wadaiwa katika wilaya hizo wanatakiwa kulipa deni la Sh7 bilioni.

Amebainisha kuwa changamoto zinazowakabili wakusanya kodi kutoka kwenye ofisi hiyo ni pamoja na watu kutokuwa na utayari wa kutekeleza takwa hilo kwa mujibu wa sheria.

Pamoja na changamoto hizo wapo wanaothamini suala hilo na wanalipa kodi kwa hiari yao huku wale ambao hawatii wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live