Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbaroni kwa kujifanya Usalama wa Taifa

Pingu 1024x769 Polisi imekua ikiwatia mbaroni wahalifu wanaojifanya watumishi wa Umma

Mon, 30 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia mwanamke mmoja Lucy Mwaipopo kwa tuhuma za kujifanya afisa usalama wa Taifa ili kutapeli mamilioni ya fedha za wananchi huku akiwaahidi kuwasaidia kutatua migogoro ya ardhi.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutumia cheo hicho kutapeli watu katika maeneo mbalimbali ikiwemo mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dar es Salaam na Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi amesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa tangu Mei 17 mwaka huu akiwa na nyaraka za watu mbalimbali aliokuwa anawalaghai kuwasaidia matatizo yao.

“Ni kweli mwanamke huyo tunaendelea kumshikilia kwa tuhuma za utapeli kwenye maeneo mbalimbali na kwamba upelelezi unaendelea ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka,” amesema Ng’anzi.

Uhalifu wa kifedha ni miongoni mwa matukio ambayo yamekuwa yakiratibiwa na baadhi ya watu nchini ambao wanataka kujipatia fedha kinyume cha sheria ikiwemo kughushi nyaraka, huku Serikali ikiendelea kudhibiti vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu za Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani ya Januari hadi Desemba 2020, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Jeshi la Polisi inaonyesha kuwa makosa ya uhalifu wa kifedha yamepungua hadi 905 mwaka 2020 kutoka makosa 1,218 mwaka 2019.

Hiyo ni sawa na kusema makosa hayo yamepungua kwa asilimia 25.7 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Wakizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) baadhi ya wananchi waliotapeliwa fedha zao wamesema walirubunika kutokana na kuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu.

Lazaro Magera ni miongoni mwa wananchi 60 ambao walitapeliwa zaidi ya Sh16 milioni, fedha ambazo walichanga ili kumpatia Lucy awasaidie kutatua mgogoro wa viwanja vyao vilivyopo Rock City Mall na Bwiru ambavyo wameingia na Serikali takribani miaka saba.

Amesema kati ya wananchi hao wapo ambao wanadai fidia ya zaidi ya Sh900 milioni kutoka halmashauri ya jiji na Manispaa ya Ilemela.

“Kutokana na changamoto hizo mwanamke huyo mwishoni wa mwezi wa tatu alidai kuwa yeye ni afisa usalama wa Taifa na anaweza kuzungumza na viongozi wa juu kutatua mgogoro huo na baada ya kumwamini alikuwa anaomba fedha za nauli na mahitaji mengine ili zimsaidie kufika huko kwa viongozi wa juu kutafuta suluhu,” amesema Magera.

Magera amedai kuwa baada ya kumbana kwa maswali mengi na wananchi kusubiri kwa muda mrefu ahadi zake hazitimii gafla alizuia mawasiliano yao na katika kumfuatialia wakagundua hakuwa afisa usalama.

Hata hivyo, kabla ya kutoroka nchini, Lucy alikamatwa na polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live