Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazungumzo kigogo wa Jaruma, DPP, TRA yaendelea

Kesi.webp Mazungumzo kigogo wa Jaruma, DPP, TRA yaendelea

Wed, 6 May 2020 Chanzo: --

UPANDE wa utetezi katika kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Jaruma General Supplies Ltd, Lucas Mallya na wenzake watano, umedai mahakamani kwamba umemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) bado wanaendelea na majadiliano.

Mallya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 23 ya uhujumu uchumi ikiwamo kukwepa kodi ya vileo, kuisababishia serikali hasara na kutakatisha zaidi ya Sh. bilioni 31.48.

Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Issaya.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa upelelezi wake bado haujakamilika aliomba tarehe nyingine ya kitajwa.

Wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo alidai kuwa wameandika barua kwenda kwa DPP na TRA ya kukiri makosa na bado wanaendelea na mazungumzo.

Hakimu Isaya alisema kesi hiyo itatajwa Mei 20, mwaka huu. Mallya na wenzake wote wanadaiwa kusababisha hasara jumla Sh. 31,489,529,153.07.

Wankyo aliwataja washtakiwa kuwa ni, Happy Mwamugunda, Prochesi Shayo, Geofrey Urio, Mhasibu Tunsubilege Mateni na Mkaguzi wa hesabu, Nelson Kahangwa.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Januari 2015 na Januari 7, 2020 jijini Dar es Salaam kwa pamoja waliongoza genge la uhalifu kwa nia ya kupata faida.

Ilidaiwa katika shtaka la pili mpaka la saba linamkabili Mallya anadaiwa Juni 3, 2019, jijini Dar es Salaam alighushi kutengeneza stempu ya ushuru akionyesha imetengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati si kweli.

Ilidaiwa kuwa alitoa nyaraka hiyo ya kughushi TRA akionyesha ni halali wakati akijua si kweli na katika shtaka lingine inadaiwa Januari 7, mwaka huu, Chang'ombe A, Temeke, jijini Dar ea Salaam alikutwa na lora 93 za stempu zenye thamani ya Sh. 80,516,000 alizochapisha bila kibali cha Kamishna wa Mapato.

Awali, kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa tisa na mashtaka 28, lakini washtakiwa watatu, Emmanuel Peter, Prokolini Shayo na Nyasulu Nkyapi, waliachiwa na mashtaka matano kuondolewa baada ya kukiri makosa yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).

Chanzo: --