Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili walalamikiwa kwa hakimu kikwazo kesi rushwa

MAHAKAMA Mawakili walalamikiwa kwa hakimu kikwazo kesi rushwa

Mon, 1 Jun 2020 Chanzo: --

MAWAKILI wa washtakiwa watatu akiwamo mfanyabiashara maarufu jijini Arusha, Shabiby Virjee (34), wanaotuhumiwa kutoa rushwa ya Sh. milioni 10, wanatuhumiwa kufanya njama za makusudi kuzuia kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu bila ya sababu za msingi.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hamidu Simbano na mwenzake Richard Jacopiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi Martha Mahumbuga wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Walidai kesi hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa Februari 8 mwaka huu, baada ya upelelezi kukamilika na watuhumiwa hao kusomewa maelezo ya awali siku hiyo, lakini ilishindikana kuanza kusikilizwa, baada ya wakili Gwakisa Sambo wa mshtakiwa wa kwanza (Virjee), kutoa sababu za kuahirisha kesi hiyo ambazo hazikuwa za msingi.

Wakili Hamidu alimweleza Hakimu Mahumbuga kuwa, washtakiwa wana mawakili zaidi ya watatu, lakini wanashindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo pale mmoja wao anapopata udhuru hasa Wakili Sambo, jambo ambalo siyo sahihi.

“Kila mara Sambo amekuwa akitoa udhuru kwa zaidi ya mara tatu wakati wako hapa mawakili wengine ambao wanaweza kumshikia wakili huyo na kesi kuendelea kusikilizwa,” alidai Wakili Hamidu.

Aidha, Wakili Hamidu alimwomba Hakimu Mahumbuga kukemea tabia hiyo na kutoa ahirisho la mwisho ili kesi hiyo isiendelee kucheleweshwa kwa makusudi na iendelee kusikilizwa.

Wakijibu hoja hiyo, mawakili wa washtakiwa hao akiwamo Godluck Maico, walikiri kuchelewesha kesi hiyo na kuahidi hali hiyo kutojirudia tena.

“Mheshimiwa Hakimu, tunaomba utusamehe kwa hili na endapo ikijitokeza siku kesi itakapopangwa kusikilizwa, itabidi ianze kusikilizwa, hivyo hivyo na sio vinginevyo kama ilivyojitokeza siku zote,” alisema Wakili Godluck.

Baada ya hoja za pande mbili kumalizika, Hakimu Mahumbuga aliwataka mawakili wote kijipanga kwa usikilizwaji wa kesi hiyo Julai Mosi, mwaka huu na kusisitiza siku hiyo kesi haitaahirishwa kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Pia alimtaka shahidi wa kwanza katika kesi hiyo Meshack Laizer, kuwapo siku hiyo bila ya kukosa ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.

“Naahirisha kesi hii hadi Julai Mosi, mwaka huu na shahidi naomba siku hiyo uwapo mahakamani hapa, ili kesi iendelea,” alisema Hakimu Mahumbuga.

Mbali ya Virjee, walioshtakiwa wengine ni aliyekuwa askari polisi Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Paulo Erasmo (37) na mfanyakazi wa kampuni ya mafuta ya Oryx, Nenzi Pazi (38).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kutoa rushwa ya Sh. milioni 10, ili kumpatia askari polisi Meshack Laizer aliyekuwa amewakamata wafanyakazi wawili wa kampuni ya Oryx wakiuza mafuta uchochoroni Moshono kinyume cha sheria ili waachiwe.

Chanzo: --