Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili wakwamisha kesi ya vigogo TPDC

Tue, 16 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Shirika Maendeleo ya Petrol Tanzania(TPDC), James Mataragio na wenzake wanne imeshindwa kuendelea kutokana na mawakili wanaoendesha shauri hilo kupata udhuru.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa mkurugenzi wa fedha, George Seni, Welington Hudson aliyekuwa mkurugenzi wa mipango na mkakati, Kelvin Komba na aliyekuwa mkurugenzi wa manunuzi na Ugavi, Edwin Riwa.

Wakili wa Serikali, Elia Athanas amesema hayo leo Jumanne Aprili 16, 2019 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Kelvin Mhina kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya usikilizwaji.

Athanas amedai upande wa Jamhuri ulikuwa na maombi kuwa shauri hilo liahirishwe lipangiwe tarehe nyingine kwa kuwa Wakili wa Serikali wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Aneth Mavika na wakili, Oliver Bukulu amepata udhuru.

Naye wakili wa utetezi, Selemani Mponda ameiomba mahakama hiyo imruhusu mshtakiwa James Mataragio kwenda Uingereza kwa ajili ya mahafali ya mtoto wake.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mhina amemruhusu mshtakiwa huyo kusafiri na siku iliyopangwa shauri hilo kusikilizwa anatakiwa kuwepo mahakamani bila kukosa.

Hakimu Mhina ameahirisha shauri hilo hadi Mei 30, 2019 itakapokuja kwa ajili kusikilizwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi washitakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Aprili 8, 2015 na Juni 3, 2016, wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC kwa nafasi zao, wakati wakitimiza majukumu yao kwa makusudi walitumia madaraka vibaya.

Ilidaiwa walibadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa mwaka wa manunuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha airborne gravity gradiometer survey ndani ya Ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo.

Inadaiwa kitendo hicho kinakiuka kifungu cha 49(2) cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 huku ikidaiwa kwamba lengo lilikuwa ni kujipatia manufaa yasiyo halali ya Dola 3.2 milioni ambazo ni sawa na Sh7.2 bilioni.



Chanzo: mwananchi.co.tz