Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili waiangukia mahakama upelelezi kesi ya vigogo wizara ya Nishati kutokamilika

34254 Pic+uganda Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wawili wa Wizara ya Nishati, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuweka amri ndogo za ukali katika mashauri ambayo yanachukua muda mrefu kukamilika kwa upelelezi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi, Archard Kalugendo na Vito Tanzania  (Tansort) na mthamini wa madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu.

Washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande kwa muda wa mwaka moja na miezi mitatu sasa, huku upelelezi wa shauri hilo ukiwa bado haujakamilika.

Kalugendo na Rweyemamu, walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Septemba 15, 2017 kujibu shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara  ya Dola za Marekani 1,118,291.43, (Sh 2.4bilioni),  lakini upelelezi wake mpaka sasa, bado haujakamilika.

Ombi hilo limetolewa leo Jumatatu Desemba 31, 2018 na wakili wa utetezi ,Nehemia Nkonko, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Wilbard Mashauri, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na jalada halisi lipo kwa  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP).

 “Wateja wangu wamechoka kauli hii ya upande wa mashtaka kila siku upelelezi haujakamilika jalada lipo kwa  (DPP), naoimba mahakama iwe na ukali na iweke sheria ndogondogo ambazo zitawabana upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati” amedai Nkoko.

“Niseme tu, upande wa utetezi tumechoka na kauli ya upelelezi bado haujakamilika, naiomba mahakama hii, terehe nyingine waje na taarifa wamefia wapi kuhisiana na wateja wangu” amedai .

Awali, wakili wa Serikali , Elia Athanas amedai , kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na jalada halisi la kesi hiyo bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mshtaka nchini( DPP) kwa ajili ya maamuzi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mashauri aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanakuja na maelezo ya kutosha siku kesi hiyo itakapotajwa.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 14, 2019. itakapotajwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya Sh 2.4bilioni.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

Kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathaminishaji wa Almasi wa Serikali na waajiriwa wa wizara ya Madini na Nishati, waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 1,118,291.43  ambazo ni sawa na Sh2,486,397,9.

Mhutasari:

Upande wa Utetezi katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayowakabili vigogo wawili wa wizara ya Nishati, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuweka amri ndogondogo za ukali katika mashauri ambayo yanachukua muda mrefu kukamilika kwa upelelezi.



Chanzo: mwananchi.co.tz