Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili wahoji jalada kesi ya mauaji ya mwanaharakati ‘kusota’ kwa DPP

Thu, 17 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya mauaji inayowakabili washtakiwa 17, wakiwemo raia wa Burundi lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kuliandalia taarifa maalum.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, likiwemo la mauaji ya mwanaharakati wa kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo, Wayne Lotter (52),

Wakili wa Serikali, Sada Mohamed amedai leo  Jumatano Januari 16, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipotajwa.

"Jalada ya kesi hii lipo kwa DPP kwa ajili ya kuandaa taarifa muhimu, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai Sada.

Sada baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Mluge Fabian na Benedict Ishabakaki  wamedai kuwa kesi hiyo ni  ya muda mrefu na mpaka sasa upelelezi wake bado haujakamilika.

" Jalada la  kesi hii lipo kwa DPP kwa muda mrefu sasa tangu Julai 9, 2018. Tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi, wateja wetu wanaendelea kusota rumande bila kujua hatima yao" amedai Mluge.

Akijibu hoja hizo, Sada amedai  katika kipindi hicho cha Julai 9, 2018 jalada hilo lilikuwa kwa DPP kwa ajili ya mambo mengi na sio kwa ajili ya kuandaliwa taarifa, kwa sasa ndio linaandaliwa taarifa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2019.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana shtaka linalowakabili kutokuwa  na dhamana.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji Namba 19/2017 ni raia wawili wa  Burundi; Nduimana Jonas (40) na Bonimana Nyandwi.

Wengine ni Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A; Innocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini; Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na ofisa wa benki ya NBC, Robert Mwaipyana (31) mkazi wa Temeke Mikoroshini.

Washtakiwa wengine ni meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B; Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala B;  Mohammed Maganga (61) ambaye ni mchimba makaburi;  Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Ayoub Selemani, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka,  katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie iliyopo Wilaya ya Kinondoni , wanadaiwa kumuua  Lotter.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz