Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili wacharuka maelezo ya mshtakiwa

Mawakilipic Mawakili wacharuka maelezo ya mshtakiwa

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Maelezo yanayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa tatu katika kesi ya uhujumu uchumi na ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu yaliibua kesi nyingine ndogo ndani ya kesi ya msingi baada ya mawakili wa utetezi kupinga yasipokewe mahakamani.

Mawakili hao walicharuka baada ya shahidi wa nane wa Jamhuri kuiomba mahakama iyapokee kama sehemu ya ushahidi wake.

Shahidi huyo, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru (OC- CID), mkoani Arusha, Mrakibu wa Polisi (SP) Jumanne Malangahe aliieleza Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kuwa ndiye aliyeandika maelezo ya Mshtakiwa wa tatu, Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, shahidi huyo alieleza kuwa aliandika maelezo ya mshtakiwa huyo Agosti 7, 2020 katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, alikofikishwa baada ya kukamatwa mjini Moshi Agosti 5, 2020.

Alidai kabla ya kuandika maelezo yake, alimuonya mshtakiwa huyo kwa mujibu wa sheria kuwa halazimishwi kutoa maelezo isipokuwa kwa hiyari na kwamba atakachokisema kitaandikwa na kinaweza kutumika mahakamani kama ushahidi dhidi yake.

Vilevile, Jumanne alidai kuwa alimpa haki zake zote ikiwa ni pamoja na kutoa maelezo yake mbele ya mwanasheria, ndugu au rafiki na kwamba mshtakiwa aliridhia kutoa maelezo kwa hiyari bila kuwepo mtu mwingine.

Aliiambia mahakama kuwa baada ya kuandika maelezo alimpa mtuhumiwa ayasome na baada ya kuridhika nayo mshtakiwa huyo alitia saini yake.

“Naiomba Mahakama iyapokee maelezo haya yawe sehemu ya ushahidi wangu,” alisema SP Jumanne baada ya kuulizwa na Kidando angependa mahakama iyafanyeje maelezo hayo.

Kufuatia ombi hilo, mawakili wa utetezi waliamka na kuyapinga maelezo hayo, mmoja baada ya mwingine, huku wakili John Mallya akitumia maneno makali ya kuituhumu Jamhuri kwa kudanganya.

Tuhuma hizo ziliwaibua mawakili wa Serikali waliopinga tuhuma hizo kiasi cha Jaji Joachim Tiganga kumtaka Mallya asitumie maneno makali.

Hoja za kupinga maelezo

Wa kwanza kupinga maelezo hayo alikuwa wakili wa Ling’wenya, Fredy Kihwelu aliyetoa sababu tano kisha akaungwa mkono na mawakili wengine wa utetezi.

Katika sababu ya kwanza, Kihwelu alidai kuwa Ling’wenya hajawahi kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, wala kuandika maelezo hayo tarehe hiyo ya Agosti 7, 2020 au siku nyingine yoyote.

Pili, alidai mteja wake alitakiwa tu kutia saini maelezo yaliyokuwa yameshaandaliwa katika Kituo cha Polisi Mbweni wala hakupewa haki ya kuyasoma.

Pia Kihwelu alidai Ling’wenya alitishiwa kwa bastola na Inspekta Mahita na SP Jumanne Malangah kuwa mateso aliyoyapata Moshi yataendelea asiposaini.

Katika sababu nyingine, Kihwelu alidai maelezo yanayodaiwa kuwa ya Ling’wenya yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria, yaani baada ya sasa nne kupita tangu alipokamatwa.

Katika sababu ya nne wakili Kihwelu alidai kuwa maelezo hayo yamerekodiwa chini ya sheria isiyokuwepo, yaani marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ya mwaka 2018.

Mwisho, alidai kuwa mshtakiwa alionywa chini ya sheria isiyo sahihi. Kwa upande wake, Mallya alidai kwenye kabrasha walilopewa na mahakama kwenye maelezo ya Ling’wenya inaonekana katika Sheria ya Ugaidi wameongeza kifungu kidogo cha 2 cha kifungu cha 24, wakati katika maelezo ambayo yanataka kuwasilishwa kifungu hicho hakipo.

“Kwa hiyo inaonekana walitudanganya washtakiwa na sisi mawakili wao,” alidai Mallya.

Alidai njia pekee ya kushughulikia uongo huo wa wazi ni kuufanya uwe faida kwa washtakiwa kwa kukataa yasipokewe kama kielelezo na kwamba mahakama iamuru kuwa hatua ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi iliyofanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu haikuwa halali.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla alipinga tuhuma hizo alizoziita nzito ambazo hazina ushahidi, akidai kuwa hizo ni nyaraka ambazo zina maandishi na kwamba anatakiwa kueleza kuwa hizi nyaraka zinatofautiana nini.

Hilla alidai kuwa ipo namna nzuri ya kushambulia nyaraka inayokubalika kisheria na akaiomba mahakama imwelekeze Mallya.

Baada ya maelekezo, Mallya aliendelea na hoja nyingine akidai kuwa kwa mujibu wa uso wa nyaraka hiyo maelezo hayo yamechukuliwa chini ya Sura ya 20 ya Marekebisho ya Mwaka 2018 ambayo haipo.

“Hii inawaathiri wateja wetu, zoezi lililozaa nyaraka hii ni zoezi la kisheria na inapaswa kufuata misingi ya kisheria. Kutaja sheria ambayo haipo nchini ni kutokukidhi matakwa ya kisheria.”

Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai katika maelezo wanayoyapinga hakuna onyo kwa sababu onyo limekusudiwa kupelekwa kwa Ling’wenya kwa kifungu cha 24 ambacho hakina kifungu kidogo. “Kifungu hiki kinaunda Makosa mawili. Kifungu cha 24 (1) ni onyo la kula njama kutenda vitendo vya ugaidi nje ya Tanzania na 24 (2) ni onyo la kula njama ndani ya Tanzania. Kwa hiyo, aliyeonywa hajui kama anaonywa kutenda vitendo vya ugaidi nje au ndani Tanzania,” alisema Kibatala na kuongeza:

“Lakini pia ameonywa kwa sheria ambayo haipo. Imetamkwa kuwa Sheria ya Kupambana na Ugaidi lakini sheria tuliyo nayo kwa Kiingereza inaitwa Prevetion of Terrorist (kuzuia gaidi) na si Combating terrorism (kupambana na ugaidi).” Naye Wakili Nashoni Nkungu alidai kuwa nyaraka hiyo haijakidhi vigezo vya kuwa maelezo ya onyo.

Alidai kuwa chini ya kifungu cha 57(2) (b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), mara tu anayehojiwa anapoanza kukiri, hutakiwa kupewa onyo la pekee na ndipo linapokuja hitaji la kumuita mlinzi wa amani.

“Kutokana na kuonywa kwa ujumla tu kwa kifungu cha 24 cha Sura ya 19, mteja wetu naye amekubali kuonyeka kwa kifungu hicho kisicho halali na hizo ndizo athari zake kwa kuonywa kwa kifungu kisicho halali.”

Akijibu, Kidando alisema katika mapingamizi hayo kuna ambayo yamejikita kifungu cha 27 cha Sheria ya Ushahidi na yale ambayo yamejikita kwenye kutokukidhi matakwa ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

“Kiutaratibu aina hizo za mapingamizi zilitakiwa zichukuliwe kwa namna mbili. Kutokukidhi matakwa ya CPA, mawakili wa pande zote mbili tulitakiwa kutoa hoja na mahakama itoe uamuzi na yale ya Sheria ya Ushahidi yalitakuwa trial within trial (Kesi ndani ya kesi ya msingi),” alisema Kidando na kuongeza:

“Sasa kama mheshimiwa jaji utaridhika basi trial within trial iwe conducted (iendeshwe) na itakapokamilika tutatoa hoja kuhusu masuala yale ya kutokukidhi matakwa ya CPA.

Jaji Tiganga alikubaliana na maombi hayo na kuamuru kuendelea kwa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi leo saa 5:00 asubuhi.

Chanzo: mwananchidigital