Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili wa Sabaya wavutana na afisa wa TAKUKURU

1dad051263f9b7ac43311471344c0c9a.jpeg Mawakili wa Sabaya wavutana na afisa wa TAKUKURU

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHAHIDI wa nane katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya {34} na wenzake sita amesema hawezi kueleza kilichomo kwenye video sita alizokabidhi mahakamani kwa kuwa si kazi yake.

Shahidi huyo, John Kisaka (35) alisema jana kuwa yeye alikuwa na kazi ya kuchunguza mfumo wa kamera za CCTV za benki ya CRDB tawi la kwa Mrombo jijini Arusha na si vinginevyo.

Kijana huyo ni Ofisa Uchunguzi wa Maabara ya Kiuchunguzi ya Kieletroniki TAKUKURU Upanga, Dar es Saalam.

Aliileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kuwa, baada ya kumaliza kazi hiyo alikabidhi kwa ofisa uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, Ramadhani Juma ambaye ni mtaalamu wa kuzitafsiri video hizo.

Kwa mujibu wa Kisaka, Juma anafanya kazi idara ya uchunguzi Takukuru Arusha.

Wakati akihojiwa na wakili Mosses Mahuna anayemtetea Sabaya alidai kuwa alichunguza tukio la Januari 22 mwaka huu katika benki hiyo na Mei 31 mwaka huu alikabidhi taarifa.

Mahuna alimtaka aeleze kuhusu watu waliokuwa katika video hiyo akasema hawezi kutafsiri taarifa ya video hizo sita zilizorekodiwa benki kwa sababu si kazi yake.

Kisaka alisema Juma atakwenda mahakamani hapo kueleza kila mmoja aliyekuwepo katika video hiyo siku hiyo Januari 22 mwaka huu kuanzia saa 10.09 jioni hadi saa 11 .05 jioni.

Alidai kuwa alikwenda Arusha na vifaa vya kazi vya kiuchunguzi na kupewa kibali na mkuu wake wa idara na aliifanya kazi hiyo kwa umakini hivyo mengine hayafahamu kwa kuwa si majukumu yake katika kazi aliyopewa.

Kisaka alisema alichokabidhi yeye kilitoka kwenye mfumo wa kamera za CCTV za benki hiyo na kwamba vingine vilibaki katika mfumo wa benki hiyo kwa kuwa alikuwa havihitaji.

Alidai kuwa baada ya kumaliza uchunguzi alijaza fomu 29 yenye kuonesha makabidhiano na ofisa uchunguzi Takukuru Arusha na aliondoka Arusha hivyo hafahamu chochote kuhusu kesi hiyo.

Apohojiwa na wakili Fridolini Bwemelo anayemtetea mshitakiwa wa tano, sita na saba Kisaka alidai kuwa katika taarifa yake kuhusu video hizo sita hakumtambua yeyote ila aliona watu wakiingia na kutoka katika benki hiyo wakipata huduma za kibenki ikiwa ni pamoja na kuweka na kutoa fedha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz