Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili kesi ya ‘Mpemba’ aliyetajwa na JPM wacharuka

34527 Pic+kesi Tanzania Web Photo

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake,  umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuchoshwa na maelezo ya upande wa mashtaka kuwa jalada la shauri hilo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Wakili wa utetezi, Hassan Kiangio ameieleza mahakama hiyo  leo Jumanne, Januari 2, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Wanjah Hamza baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa DPP kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Yusuf na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande kwa miaka miwili na mwezi mmoja sasa kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Washtakiwa hao walifikishwa Kisutu mara ya kwanza, Novemba 17, 2016 kujibu mashtaka yanayowakabili.

"Kesi hii ni ya muda mrefu, wateja wangu wanaendelea kusota rumande bila kujua hatima yao. Tumechoshwa na hizi kauli za upande wa mashtaka kuwa jalada lipo kwa DPP linafanyiwa kazi,  tunataka watuambie wamefikia wapi juu ya upelelezi wa kesi hii,” amesema Kiangio.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali,  Elia Athanas  amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba jalada halisi la kesi hiyo lipo kwa DPP hivyo wanasubiri uamuzi wake.

"Tunasubiri uamuzi kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini  kwa sababu jalada hili lipo katika ofisi yake kwa ajili ya kulipitia na kulitolea uamuzi,” amedai Athanas.

Hata hivyo, Novemba 15, 2018 wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliieleza mahakama hiyo kuwa wapo katika hatua za mwisho za uandaaji wa nyaraka ili kuipeleka kesi hiyo katika hatua nyingine.

Hakimu Hamza baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 15, 2019 itakapotajwa  tena.

Amesema hoja za upande wa utetezi zitafanyiwa kazi na hakimu anayesikiliza shauri hilo, Thomas Simba atakaporudi kutoka likizo.

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika tarehe tofauti kati ya Januari 2014 na Oktoba 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, washtakiwa walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 180,000 za Marekani sawa na Sh392.8milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.



Chanzo: mwananchi.co.tz