Dar es Salaam. Mawakala kumi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa matatu likiwemo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh10.87 milioni kwa lengo la kuwakatia watu tiketi za ndege za shirika hilo.
Akisoma hati ya mashtaka leo Jumatatu Desemba 24, 2018 Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salum Ally amedai washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye makosa matatu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Fabian Ishengoma, Adamu Kamara, Marlon Masubo, Alexander Malongo, Tunu Kiluvya, Jobu Mkumbwa, Mohamed Issa, Godfrey Mgomela, Absalom Nyusi na Janeth Lubega.
Wakili Simon amedai katika shtaka la kwanza washtakiwa hao wanadaiwa kuisababishia hasara shirika la ATCL.
Amedai katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na Oktoba 9,2018 wakiwa maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam na mkoa wa Mwanza watuhumiwa hao waliisababishia shirika hilo hasara ya Sh10.87 milioni huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.
Katika shtaka la pili tarehe tofauti kati ya Machi 10 na Oktoba 9, 2018 wa katika mkoa wa Dar es Salaam na mkoa wa Mwanza watuhumiwa hao walitumia njia ya udanganyifu kujipatia kiasi cha Sh 10.87 milioni kwa lengo la kuwakatia watu tiketi za ndege la shirika hilo .
Amedai katika shtaka la tatu la utakatishaji wa fedha katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na Oktoba 9, 2018 wakiwa katika mkoa wa Dar es Salaam na mkoa wa Mwanza wstuhumiwa hao walijipatia Sh10.87 milioni ni mali ya shirika la ATCL huku wakijua ni kosa la kisheria
Baada ya kuwasomea mashtaka hayo Wakili Simon amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo kunaomba tarehe nyingine kwaajili ya kutajwa.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo Hakimu Ally amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa sheria na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 7,2019.