Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakala 12 wa ATCL jela miaka 20 baada ya kushindwa kulipa faini

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu mawakala 12 wa Shirika la Ndege Tanzania  (ATCL) kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja au kwenda jela miaka 20 baada ya kukiri shtaka la kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh10.8 milioni.

Mbali na faini hiyo, washtakiwa wameamriwa kulipa fidia ya Sh10.8 milioni kwa pamoja.

Washtakiwa hao wameshindwa kulipa faini na fidia na kupelekwa gerezani ambako kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Mahakama hiyo imesema vifaa vilivyotumika kusababisha hasara hiyo ambavyo ni simu 13 na kompyuta sita vitaifishwe na kuwa mali ya Serikali ya Tanzania.

Akitoa hukumu hiyo leo Jumatatu Septemba 2, 2019 hakimu mkazi mwandamizi, Salum Ally amesema amewatia hatiani washtakiwa hao baada ya kukiri shtaka lao la kuisababishia hasara ATCL.

Hakimu Ally amesema amezingatia hoja zilizotolewa na pande zote mbili, amewatia hatiani washtakiwa hao kama walivyoshtakiwa.

Pia Soma

Advertisement   ?
Washtakiwa hao katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 97/2018  ni Fabian Ishengoma, Adamu Kamara, Marlon Masubo, Alexander Malongo, Tunu Kiluvya, Jobu Mkumbwa, Mohamed Issa, Godfrey Mgomela, Absalom Nyusi, Janeth Lubega, Mary Semakweli na Janet Lubega.

Mawakala ATCL waendelea kusota rumande

Awali,  wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania( DPP) ametoa kibali cha kuiruhusu Mahakama ya Kisutu kusikiliza shauri hilo.

Wakili Simon baada ya kueleza hayo aliwasomea washtakiwa hao shtaka linalowakabili.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka lao walikiri kutenda kosa hilo na mahakama imewatia hatiani na kutoa hukumu.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili Simon aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwao na kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

"Naiomba mahakama iamuru Laptop (Kompyuta mpakato) na simu za mkononi zilizotumika kuisababishia Serikali hasara zitaifishwe na kuwa  mali ya Serikali. Naiomba mahakama iamuru washtakiwa hawa kulipa fidia ya hasara waliyoisababishia ATCL,” amedai wakili Simon.

Wakili wa utetezi,  Benedict Ishabakaki amedai washtakiwa hao ni wakosaji wa kwanza na kwa kuwa wamekiri mashtaka yao wenyewe anaiomba mahakama iwapunguzie adhabu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi 3 na Oktoba 9, 2018 katika maeneo tofauti kati ya Dar es Salaam na Mwanza, waliisababishia  ATCL hasara ya Sh10,874,280.

Chanzo: mwananchi.co.tz