Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya wanawake, watoto yawaibua Tamwa

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimelaani na kukemea vikali matukio ya mauaji ya wanawake na watoto yaliyotokea hivi karibuni hapa nchini.

Pamoja na matukio ya mauaji ya watoto yaliyoripotiwa kutokea mikoa ya Njombe na Simiyu, kumetokea mauaji ya wanawake katika mkoa wa Arusha na mingine.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben iliyotolewa leo Ijumaa Februari 22, 2019, chama hicho kinawataka wadau wengine kuanzia ngazi ya familia hadi Serikali kuwalinda watoto na kumaliza migogoro ya kifamilia kwa amani.

“Tamwa tunasikitishwa na mauaji hayo na tunaikumbusha jamii kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi kulingana na sheria na taratibu za nchi yetu,” alisema Rose na kuongeza;

“Tumeona na tunapongeza juhudi zilizofanywa na vyombo vya usalama nchini japo pamoja na juhudi hizo cha kujiuliza ni kuwa kwa nini bado matukio haya ya mauaji yameendelea kuripotiwa siku baada ya siku?”

Mkurugenzi huyo wa Tamwa amesema matukio hayo yasipoundiwa mifumo ya muda mrefu ili kuyakomesha kabisa, wanawake na watoto ambao ni nguvu kazi ya Taifa wataendelea kupotea.

Ameshauri kuwepo kwa mfumo endelevu utakaohusisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi, vyombo vya usalama na kampuni za simu kuwezesha waathirika kutoa taarifa za dalili zozote za ukatili kabla haujatokea.



Chanzo: mwananchi.co.tz