Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya vikongwe Geita yapungua 95%

5f9c6125e08d6bf580da853b03d02c52 Mauaji ya vikongwe Geita yapungua 95%

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHi la Polisi Mkoa wa Geita limesema hadi sasa juhudi za kumaliza mauaji ya vikongwe kwenye mikoa ya kanda ya ziwa zimefanikiwa kwa takribani asilimia 95.

Kwa mujibu wa Kamanda Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe (pichani) mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamemalizika kwa asilimia 99 hadi 100.

Kamanda Mwaibambe alisema hayo wiki iliyopita wakati akizungumza na gazeti hili na kueleza sababu kubwa ya kupungua kwa matukio ya aina hiyo ni juhudi zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutoa elimu iliyosaidia kuondoa imani potofu iliyokuwa kiini cha mauaji hayo.

Alisema elimu kwa wananchi imeongeza molari ya wao kushirikiana na Jeshi la Polisi na kwamba, hivi sasa kukiwa na vitisho ama viashiria vya mauaji ya vikongwe ama walemavu wa ngozi wamekuwa tayari kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kuwabaini wahusika.

“Jeshi la Polisi kwa sasa lina mtandao mkubwa, inapotokea mauaji ya aina hiyo lazima tuwapate wahusika na tupate majibu, tunashukuru mtandao wetu uliweza kuwabaini wauaji wanaofanya kazi hiyo kwa kukodiwa maarufu kama “Hard Killers” tumewakamata wengine wanasema walikuwa na kazi Kigoma wanalipwa elfu 30 hadi elfu 40 lakini tumewadhibiti,” alisema Kamanda Mwaibambe.

Mkuu wa Mkoa wa Geita , Robert Gabriel alisema chanzo kingine cha mauaji ya vikongwe na walemavu ilikuwa ni upungufu wa huduma bora za afya uliokuwepo kwani jamii ilijikita zaidi katika tiba za jadi na imani za kishirikina hivyo maboresho ya huduma za afya yaliyofanywa na serikali imesaidia jamii kubadilisha mtazamo huo.

Alisema awali kabla ya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya vya kutosha, watu wengi walipougua kimbilio lao lilikuwa ni kwa waganga wa kienyeji ndiyo maana waliaminishwa ushirikana na kuishia kutenda matukio hayo lakini leo hii baada ya kuboresha huduma za afya na elimu jamii imeelimika na kuachana na dhana potofu.

Mapema mwezi huu akiwa ziarani mkoani Geita Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama nchini kwa kufanikiwa kumaliza matukio ya mauaji ya vikongwe na walemavu hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa.

Alisema miaka kadhaa ya nyuma mikoa ya kanda ya ziwa ilikuwa inakabiliwa na tatizo hilo lakini sasa imebaki historia baada ya serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa imara kukabiliana na matukio hayo.

Chanzo: habarileo.co.tz