Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya raia yamuibua IGP

WAMBURA IGP UOELKEKEZI Mauaji ya raia yamuibua IGP

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Kufuatia mauaji ya watu wawili na wengine tisa kujeruhiwa baada ya askari wa Jeshi la Polisi kudaiwa kuwarushia risasi na mabomu ya machozi wilayani Kilombero, mkoani Morogoro, Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Camillius Wambura ameunda timu ya uchunguzi wa tukio hilo sambamba na kuwasimamisha baadhi ya maofisa na askari wa jeshi hilo.

Kuundwa kwa timu huru ya uchunguzi chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na taasisi nyingine za Serikali, kulitangazwa jana na IGP Wambura ikiwa ni siku moja tangu kutokea kwa tukio hilo linaloelezwa kuwa lilitokana na vurugu zilizofanywa na wakulima.

Wakulima hao walilamikia kitendo cha wafugaji kuingiza mifugo katika mazao na wenzao wawili kushambuliwa Oktoba 22, 2022.

Jambo hilo lilifanya wakulima hao kujichukulia sheria mkononi kwa kuwakamata viongozi wa kijiji hicho cha Ikwambi pamoja na mkaguzi wa kata na kuwafungia katika ofisi ya kijiji, kabla ya polisi kufika eneo hilo ili kuwaokoa wakidaiwa kutumia nguvu kubwa.

Hatua za IGP

Katika taarifa yake kwa umma, IGP Wambura alisema: “Kutokana na tukio hilo, timu maalumu imeundwa chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa Mashtaka na taasisi nyingine za Serikali kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi huru utakaowezesha kupata majibu ya chanzo cha tukio na kikubwa ni kubaini uwiano wa matumizi ya nguvu iliyotumiwa na Jeshi la Polisi katika kudhibiti vurugu hizo....’’

Ili kuipa uhuru timu hiyo kufanya kazi yake, alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha askari wote waliohusika katika tukio hilo wanakaa kando kupisha uchunguzi.

“Hii itafanya timu hii huru iwe na nafasi nzuri na njema iweze kutimiza wajibu wake na kuja na majibu na matokeo sahihi ya uchunguzi huo kwa jamii ili Watanzania waweze kufahamu ukweli wa tukio hilo na kama nguvu zilizotumika zinaendana na tukio hilo,” ilisema taarifa yake na kuongeza:

“Na endapo kutabainika upungufu, udhaifu au chochote kinachoonyesha uzembe kwa yoyote, basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati timu ikifanya kazi yake ya uchunguzi, huku akiliagiza Jeshi la Polisi mkoani Morogoro hasa wilaya ya Kilombero, kutoa ushirikiano kwa timu inayokwenda kufanya uchunguzi ili ukweli ubainike.

Chanzo cha vurugu

Vifo hivyo vilitokea Oktoba 23, majira ya mchana kufuatia vurugu na hivyo kuwalazimu askari kuwarushia risasi na mabomu ya machozi wananchi wa Kijiji cha Ikwambi waliokuwa wakiandamana kupinga mashamba yao kulishwa mifugo.

Akizungumza jana katika mkutano ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatuma Mwasa, Mwenyekiti wa kijiji cha Ikwambi, Bleckimanzi, alidai kuwa wananchi wamekuwa wakipeleka malalamiko ya mashamba yao kuingiliwa na mifugo ya wafugaji, lakini polisi wamekuwa wakipuuza.

Aliwataka wananchi kuwa watulivu huku hatua mbalimbali za kiuchunguzi zikiendela kuchukuliwa.

Alisema Serikali inatoa rambirambi kwa familia za marehemu kiasi cha Sh2 milioni kwa maana ya kila familia kupata Sh1 milioni.

Waliokufa wametajwa kuwa ni Ally Msoma (49) na Asha Kilamilo (72) ambao maiti za marehemu hao zilikabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za maziko ambayo yamefanyika jana.

Marehemu Asha Kilamilo (72) amezikwa katika kijiji kwao kata ya Namawala, huku marehemu Ally Msoma akizikwa kata ya Mofu.

Mkazi wa Ikwambi, Clence Mtaalamu alisema mgogoro wa wakulima na wafugaji ni tatizo ambalo lilifumbiwa macho muda mrefu, kwani wafugaji wamekuwa wakivamia mashamba na ng’ombe kula mazao ya wakulima, huku wakiwashambulia wakulima kwa viboko.

Mtaalamu alisema wakulima walipokuwa wakifanya hivyo walikuwa wakipeleka malalamiko kituo cha Polisi Kata, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Mkazi mwingine, Coleta Mmala aliiomba Serikali kuweka ulinzi wa kutosha kwenye maeneo ya wafugaji na wakulima ambapo pameanza kuwapo kwa sintofahamu kati yao.

Mmala alitaja maeneo yanayoonyesha viashiria vya kuwepo kwa migogoro ya wakulima na wafugaji kuwa ni baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kilombero, Wilaya ya Morogoro (DC) Ulanga, Kilosa na Malinyi, huku akisema hatua zisipochukuliwa hatari zaidi inaweza kutokea.

Baba wa marehemu anena

Baba wa marehemu Ally Msoma, Idd Msoma akizungumzia tukio hilo alisema yeye alipata taarifa ya mtoto wake kupigwa risasi akiwa shambani na aliporejea alikuta mwili wa mtoto wake ukiwa chini umefunikwa.

Aliwatuhumu polisi kwa mauaji hayo na kwamba kama wasingetumia nguvu watu wasingeuawa na kifo cha mtoto wake ni baada ya viongozi wa kijiji kutoshughulikia matatizo ya wananchi, ambao waliamua kuandamana na kufanya walichokifanya.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wanakijiji waliozungumza kwa simu jana na Mwananchi walisema tatizo la mgogoro wa wakulima na wafugaji lilianza mwaka 2021 na mpaka kufikia sasa na kwamba mgogoro huo umeonekana kutuchukuliwa hatua yoyote na ngazi hizo.

Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Ikwambi Victory Timbulu alisema:

“Watu wamekuwa wakifika kituo cha Polisi kulalamika lakini hakuna lolote linalofanyika hakuna kupelekwa mahakamani, watu wanaendelea kuuawa, kupigwa viboko sasa wananchi wamekaa na vitu hivi kwa muda mrefu bila kupata msaada na kuhamua kujichukulia hatua hizo,” alisema Timbulu.

Mauaji wakulima, wafugaji

Vurugu hizo zimetokea ukiwa umepita mwaka mmoja tangu zitokee vurugu nyingine za wakulima na wafugaji wilayani Kilosa mkoani humo, ambapo mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la John Nyerere kufariki na wengine wanne kujeruhiwa.

Mauaji hayo yalitokea baada ya wafugaji wa jamii ya Kisukuma kuwatuhumu wafugaji wenzao wa Kimasai kutaka kuiba mifugo yao.

Kufuatia mauji hayo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela (sasa Mkuu wa Mkoa wa Geita), akiongozana kamati yake ya Ulinzi na usalama ya mkoa walifika katika kijiji hicho na kuagiza wote waliohusika kukamatwa.

Chanzo: mwanachidigital