Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya mapenzi yaongoza 2020

C6cdca79aa8bdba514233d80571bbf43 Mauaji ya mapenzi yaongoza 2020

Tue, 22 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMISHNA wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Liberatus Sabas, amesema kwa kiasi kikubwa mauaji yaliyotokea hapa nchini kwa mwaka huu, yanatokana na wivu wa mapenzi.

Vifo vinavyofuatia ni vya ajali, ambapo katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, kati ya ajali 1,800 zilizotokea, ajali 935 zilisababisha vifo vya watu 1,158 na majeruhi 2,089.

Mbali na mauaji, alisema makosa ya uhalifu wa kutumia silaha ukiwemo ujambazi na unyang’anyi, yamepungua kwa mwaka huu kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Sabas alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu kulikuwa na makosa 273 ya uhalifu wa kutumia silaha, ikilinganishwa na makosa 378 ya mwaka jana kwa kipindi kama hicho, ambapo tofauti yake ni makosa 105 sawa na asilimia 27. Kamanda Sabas aliyasema hayo jana kupitia taarifa yake ya matukio ya mwaka 2020 kwa vyombo vya habari.

Alisema mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi, yanatokana na msukumo wa wananchi kujichukulia sheria mkononi. Alitoa mwito kwa viongozi wa dini, kuingilia kati hali hiyo kwa kutoa elimu ili kupunguza mauaji hayo yanayotokana na wivu wa mapenzi, kwa kuwa wengi na waumini wa madhehebu mbalimbali.

“Kwa upande wa ajali za barabarani kwa mwaka huu kuanzia Januari hadi Novemba yalikuwa 1,800, kati ya hizo ajali za vifo zilikuwa 935 na waliokufa ni 1,158 na majeruhi 2,089,”alisema Sabas.

Alisema katika kipindi cha mwaka jana kuanzia Januari hadi Novemba, matukio ya ajali yalikuwa 2,722 ambapo ajali zilizosababisha vifo zilikuwa 1,117, waliokufa ni 1,329 na majeruhi ni 2,717.

Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, takwimu hizo zinaonesha kuwa kati ya mwaka jana na mwaka huu, tofauti ya matukio ya ajali ni 922 sawa na asilimia 33, ajali za vifo ni 182 sawa na asilimia 16.3, waliokufa ni 171 sawa na asilimia 12.9 na majeruhi ni 628 sawa na asilimia 23.1.

Kuhusu matukio ya shule kuungua moto, Kamanda Sabas alilieleza Habari- LEO kuwa sababu ambazo Jeshi la Polisi ilizibaini kutokea kwa matukio hayo ya moto kuwa ni pamoja na itikadi kali, utovu wa nidhamu, utukutu wa wanafunzi na kutofanyika kwa ukaguzi wa miundombinu ya majengo.

Hali hiyo inasababisha maswali na wasiwasi kwa wananchi, ambapo mpaka sasa jumla ya wanafunzi 32 ndiyo waliokamatwa kuhusika na matukio hayo ya moto.

“Jumla ya shule zilizoungua kutoka Januari hadi Novemba mwaka huu ni 31, shule za watu binafsi au taasisi za kidini zilikuwa 20 na shule za serikali ni 11, hii imetokana na sababu tofauti ikiwemo hitilafu ya umeme, migogoro shuleni na uzembe,”alisema.

Kamanda Sabas alisema pia kumekuwa na wimbi kubwa la wanafunzi kuacha masomo na kujiunga na makundi ya kihalifu, kama lile lililokuwa Kibiti mkoani Pwani. Alisema miongoni mwa wahalifu hao ni wale waliokuwa Kibiti, ambao walipigwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na baadaye wakakimbilia nchi jirani ya Msumbiji.

Alisema mpaka sasa kuna wanafunzi walioacha shule na kujiunga na vikundi vya kihalifu, wamekamatwa wakivuka mpaka kuelekea Msumbiji. Wengine walishafanikiwa kuvuka na wameingia nchini humo.

Aliwataka wazazi na walezi kufuatilia mienendo za watoto wao. “Wanafunzi waliokamatwa ni wawili, bado tunaendelea kuwahoji. Ni wanafunzi wa sekondari. Matukio haya yamekuwa yakijirudia.

Hata pale Arusha wapo wanafunzi walioacha chuo kimoja cha ufundi na wakawa wanaelekea Somalia, kwa hiyo ni vizuri wazazi wakaa na watoto wao karibu kwa sababu mwisho wa siku wanasema watoto wamepotea kumbe wameenda kwenye mambo ya uhalifu,”alisema Sabas.

Chanzo: habarileo.co.tz