Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya bilionea Msuya: Washtakiwa walikuja niwape kinga wasikamatwe - Mganga

Bilionea Msuyaaaa Mauaji ya bilionea Msuya: Washtakiwa walikuja niwape kinga wasikamatwe - Mganga

Thu, 7 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Agosti 7, 2023 Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Mirerani ilitikiswa na taarifa za kuuawa kwa kupigwa kwa risasi, mfanyabiashara maarufu wa madini, Erasto Msuya maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, tukio lililotokea wilayani Hai.

Katika mauaji hayo, wauaji wake waliokuwa na pikipiki walitumia mbinu ya kumshawishi kumuuzia madini ya Tanzanite na kumvuta hadi eneo la Orkolili Mijorohoni kisha walimminia risasi 22 kwa kutumia bunduki aina ya SMG.

Katika tovuti yetu jana, tulikuletea ushahidi wa shahidi wa nne wa upande wa mashtaka, Dk Paul Chaote, aliyekuwa mganga mkuu wa Hospitali ya Wilaya (DMO) ya Hai Kilimanjaro, aliyeufanyia uchunguzi mwili wa bilionea Msuya.

Alieleza kuwa, mwili wake ulikutwa na matundu 26 ya risasi, matundu madogo 13 yakiwa sehemu ambayo risasi ziliingia na matundu 13 yalikuwa ya risasi zilipotokea na zilichakaza utumbo mwembamba, kuharibu figo, mishipa ya damu na bandama.

Leo tunakuletea ushahidi wa shahidi wa tano wa Jamhuri, Khalid Sankamunge, ambaye ni mganga wa jadi, mkazi wa Kijiji cha Limbula, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, ambaye wauaji wawili walikwenda kwao kupata zindiko wasikamatwe.

Akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Neema Mwanda, shahidi huyo alisema yeye huwa anawasaidia watu kupata kinga, kuondoa mikosi na kung’arisha nyota na wateja wake wanatoka Uganda, Kenya, Burundi, Zanzibar, Congo na Tanzania.

Aliieleza Mahakama kuwa Septemba 9, 2013 akiwa nyumbani kwake Limbula, walifika vijana wawili aliowataja kuwa ni Karim (Kihundwa-mshitakiwa wa tano) na Sadick (Jabir-mshitakiwa wa sita), wakitaka awape dawa ya kinga.

“Walitaka dua ya kinga na baraka katika shughuli zao na hatimaye kuondoa nuksi. Waliponieleza habari hizo niliwaambia watulie ningezungumza nao siku iliyofuata. Hawakuwa na pesa hivyo walienda mjini ili wawasiliane na bosi wao awatumie,” alidai shahidi huyo.

Alieleza kuwa, waliporejea, walitoa Sh70,000 kwa vijana wa hapo kijijini ili wakatafuta kondoo na alipopatikana alichinjwa na kufanyiwa sadaka na kuliwa na wageni wote na akawatengenezea dawa, moja ikiwa ni ya kuogea.

Alidai kuwa, kabla ya kuwapa dawa hiyo, walimweleza kuwa huko walikotoka walikuwa wamefanya tendo la mauaji Arusha ya bilionea mmoja hivyo walikuwa wanaomba mganga huyo awasaidie pia kuwakinga na mkosi huo.

“Kwa vile nilikuwa mwenyekiti wa kijiji, nilianza kutafuta njia ya kuona namna gani watu hao wanakamatwa kwa kosa walilolifanya. Sikuwa nawafahamu, ndiyo mara ya kwanza nawaona hapo kijijini,” alieleza shahidi huyo wa tano wa Jamhuri.

Alisema Septemba 13, 2013, alipokea wageni kutoka Arusha ambao ni polisi na kumweleza walikuwa wakiwatafuta washitakiwa hao wawili wa tukio la mauaji lililotokea Arusha ambao wameelezwa kuwa wapo hapo nyumbani kwake.

“Wakati huo walikuwa wamejipumzisha chini ya mti wa mwembe. Wale vijana (washitakiwa) walipowaona tu walianza kukimbia, mmoja akikimbilia upande wa mashariki na mmoja magharibi na hilo likaniashiria kuwa ni wahalifu,” alisema.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, alisema hata hivyo, wanakijiji waliwakimbiza washitakiwa hao na kufanikiwa kuwakamata na kuwakabidhi polisi.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emanuel Safari na John Nundu walipata nafasi ya kumhoji shahidi kama ifuatavyo.

Ndusyepo: Shahidi, unajua kusoma na kuandika? Shahidi: Kusoma na kuandika naelewa. Ndusyepo: Ulipokuwa kijijini uliandika maelezo yako polisi? Shahidi: Maelezo yote yaliandikwa. Ndusyepo: Ulipoulizwa na kiongozi wa mashitaka ulisema una miaka 49. Shahidi: Ndiyo.

Ndusyepo: Ni kweli tarehe 14.09.2013 uliandika polisi una miaka 49 na leo hii una miaka 49? Shahidi: Nafuata kanuni niliyoizungumzia hapa. Ndusyepo: Hiyo kanuni umefundishwa na nani? Shahidi: Mimi mwenyewe kwa ufahamu wangu.

Magafu: Karim na Sadick walikuambia wao wanatoka Arusha? Shahidi: Kweli. Magafu: Na vilevile walikuambia mauaji ya Bilionea Msuya yalifanyika Arusha? Shahidi: Ndiyo.

Magafu: Wewe kwa utu uzima wako na hekima uliyokuwa nayo, uliwauliza ni tatizo gani lilifanya wamuue huyo mtu huko Arusha? Shahidi: Walisema wametumwa. Magafu: Hili tatizo limeshakujia wamesema wameua, wewe ulilipeleka wapi? Shahidi: Niliyaripoti ofisini kwangu kwa mtendaji wa kijiji.

Safari: Ulisema hao watu walikamatwa na wananchi, polisi walikuwa wapi? Shahidi: Polisi nguvu yao ilikuwa ndogo. Akiwa mnene atakimbia? Safari: Umeiambia Mahakama hao watu walikuwa wageni kwako, ulishawahi kuitwa popote kuwatambua? Shahidi: Sijawahi kuitwa popote ni leo.

Lundu: Wakati unaulizwa umri wako ulisema huwezi kubadilisha ulichoandika kwenye maelezo yako. Shahidi: Ni sawa. Lundu: Aliyekuambia usibadilishe ni nani? Shahidi: Siku ile nilipoandika maelezo yangu tarehe 14.9.2013 nilisema nina miaka 49, nitabadilishaje?

Kwa upande wake, shahidi wa sita, Anase Khalid ambaye ni mtoto wa mganga huyo, aliwaacha hoi wasikilizaji pale aliposhindwa kukumbuka alizaliwa lini, ana watoto wangapi na wanaitwa nani kwa majina.

Kabla ya kuchanganya huko kwa maelezo, shahidi huyo alielezea namna polisi walivyofika kijijini kwao na namna alivyoshiriki kuwakamata washitakiwa wawili, Sadick na Karim baada ya polisi kufika nyumbani kwao wakiwatafuta.

Shahidi huyo aliyekuwa akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Stella Majaliwa kutoa ushahidi wake, alisema wakati Karim akikamatwa alikuwa ameungua kwa moto kwenye mguu kwa vile alikokimbilia kulikuwa na moto.

Baada ya ushahidi wake, ndipo yalipofuata mahojiano kati ya shahidi huyo na mawakili wa utetezi kama ifuatavyo:

Ndusyepo: Uliposikia kelele zile za mwizi, ulikuta Sadick alikuwa amekamatwa baada ya muda gani. Shahidi: Sikuwa na saa siwezi kufahamu. Magafu: Unajua maana ya kuapa hapa mahakamani? Shahidi: Kwamba ushahidi wangu utakuwa wa kweli.

Magafu: Umesema Karim alipokamatwa alikuwa ameumia sehemu gani? Shahidi: Chini ya unyayo. Magafu: Nini kilisababisha akaumia? Shahidi: Alikuwa ameumia na miti wakati wa kukimbia. Magafu: Ulishawahi kuona mtu ameunguzwa na moto? Shahidi: Sijawahi.

Magafu: Umewahi kuona mtu ameumia kwa kujikwaa au kujikata na kitu au kujichoma. Shahidi: Sijawahi. Magafu: Unataka Mahakama iamini kwa umri wako wa miaka 37 hujawahi kuona mtu aliyeungua, aliyejikata au aliyejikwaa. Shahidi: Aliyejikwaa na kujikata sijawahi kumuona.

Magafu: Ni nani aliyekutajia hayo majina mawili na hukai na baba yako? Shahidi: Sadick na Karim nimewafahamu hapo hapo kijijini. Magafu: Umesema uliposikia kelele za mwizi ulikwenda na pikipiki, ni namba ngapi? Shahidi: Namba 359.

Magafu: Umesema hujasoma sasa umejuaje hizo namba? Shahidi: Mimi najua kuhesabu moja mpaka nne tu. Magafu: Kati ya nne na tisa ipi inatangulia. Shahidi: Ni vigumu kutambua. Magafu: Kati ya namba moja mpaka nne kuna namba tano? Shahidi: Sifahamu tano.

Lundu: Una watoto wangapi. Shahidi: Sijui, nina wengi. Lundu: Mtoto wako wa kwanza anaitwa nani? Shahidi: (Baada ya kufikiri kwa muda) Hamisi. Lundu: Mtoto wako wa pili anaitwa nani? Shahidi: (Baada ya kufikiri tena kwa muda) Hawa.

Lundu: Baada ya Hawa anafuata nani? Shahidi: (Baada ya kufikiri kwa muda) Inakuwa shida kukumbuka. Lundu: Kama umesahau majina ya watoto wako, kitu gani kinakufanya uwakumbuke Sadick na Karim uliowaona miaka miwili nyuma? Shahidi: Ninawafahamu. Lundu: Kitu gani kimekufanya uwakumbuke kichwani? Shahidi: Rangi zao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live