Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya Bilionea Msuya, Shahidi: Marehemu alivutwa kwa biashara ya madini

Bilionea Msuyaaaa Mauaji ya Bilionea Msuya, Shahidi: Marehemu alivutwa kwa biashara ya madini

Mon, 11 Dec 2023 Chanzo: Habarileo

Agosti 7, 2013 Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Mirerani ilitikiswa na taarifa za kuuawa kwa kupigwa kwa risasi, mfanyabiashara maarufu wa madini, Erasto Msuya maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, tukio lililotokea wilayani Hai.

Katika simulizi yetu ya jana, tuliona namna shahidi wa tisa wa upande wa mashitaka, Samwel Mwaimu aliyekuwa mkuu wa timu ya operesheni iliyohusika na ukamataji, walivyowakamata washitakiwa mbalimbali katika kesi hiyo.

Leo tutaendelea na namna timu hiyo ya ukamataji ikiongozwa na Inspekta Mwaimu, walivyoelekea Mwanza na baadaye Kigoma kwa ajili ya kumfuatilia mshtakiwa Ally Mussa Majeshi, aliyekuwa ametorokea mkoani Mwanza.

Akiongozwa na wakili Chavulla kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alieleza huko Mwanza hawakufanikiwa kumkamata Majeshi baada ya kuelezwa alikuwa ameelekea mkoani Kigoma katika harakati za kutoroka na kujificha.

Shahidi huyo alidai katika kuwafuatilia watuhumiwa, Oktoba 5, 2013 walikuwa mkoani Kigoma kumfutilia mtuhumiwa huyo na walifanikiwa kumkamata asubuhi katika kituo cha mabasi Kigoma mjini na kurudi naye kituo cha polisi.

Alieleza baada ya kurudi kituo cha polisi Kigoma mjini alifanya naye mahojiano ya awali na alikiri kuhusika na mauaji ya Erasto Msuya na kwamba Agosti 6, 2013 alikwenda hotelini kwake kujifanya kumuuza madini.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, kwa kuwa alikuwa na sampuli tu, aliondoka na kuahidiana kesho yake saa nne atamuuzia madini mengi zaidi, huku kumwambia biashara hiyo anafanya na ndugu yake.

Kulingana na shahidi huyo, alimwambia kuwa kesho yake walimpitia njia panda ya KIA wakaongozana kwenda mpaka Mjohoroni kijiji cha Orkalili wilayani Hai ambapo walimpitia Karimu na ndipo mauaii yalitokea hapo.

Hapo ndipo Wakili Emmanuel Safari alisimama na kuiambia Mahakama kuwa upande wa Jamhuri wanakiuka wanayotakiwa kufanya mtuhumiwa anapochukuliwa maelezo yatakayowasilishwa kortini na si kusema kwa mdomo.

Jaji aliieleza upande wa mashtaka wamekuwa wakichomekea vitu ambavyo vimekuwa vikikataliwa mahakamani mara kwa mara, akawataka waweke vielelezo vya msingi ambavyo vikiwasilishwa vitapokelewa.

Akimalizia ushahidi wake, shahidi huyo alidai baada ya mahojiano hayo ya awali alimkabidhi mtuhumiwa huyo kwa koplo Atway kwa ajili ya kuandika maelezo.

Sehemu ya mahojiano ya maswali ya dodoso kwa shahidi huyo na mawakili wa utetezi, Emmanuel Safari, Hudson Ndusyepo na John Lundu ni kama ifuatavyo:

Wakili Safari: Kule eneo la tukio ulikusanya risasi ngapi?

Shahidi: Jumla ya risasi zote nilizokusanya ni 30.

Wakili Safari: Umesema risasi 30 ulizozipata pale zilikuwa za aina gani?

Shahidi: Risasi za kawaida za bastola.

Wakili Safari: Nitakuwa sawa nikisema hakuna mtu yeyote ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro aliyetoa taarifa ya risasi zilizokamatwa isipokuwa wewe?

Shahidi: Siwezi kujua hilo

Wakili Safari: Je, unakubaliana na mimi kwa vile wewe ndio mkamataji na mzungumzaji wa vielelezo, hakuna mtu mwingine aliyetoa taarifa ya aina ya risasi isipokuwa wewe?

Shahidi: Sikuwa mpelelezi siwezi kujua. Hizo nilizokamata ndio hizo zimeletwa mahakamani.

Wakili Safari: (Akimpa ramani aliyoichora eneo la tukio) umehojiwa na wakili mwenzangu ukasema unapoandaa ramani unaonyesha na vielelezo, tuonyeshe ni wapi ulionyesha hivyo vitu?

Shahidi: Sikuweka mark (alama).

Wakili Safari: Wewe kama mpelelezi, ulishakutana na mambo ya kijiografia ya latitude na longitude? Kwenye ramani yako umeonyesha direction (mwelekeo)?

Shahidi: Ndio.

Wakili Safari: Ipi ina lala na barabara ya Arusha?

Shahidi: Ni latitude.

Wakili Safari: Ni latitude ngapi mpaka kwenye mwili wa marehemu ulipolala?

Shahidi: Huwezi kuziona kwa macho. Haya ni mambo ya kiupelelezi na kwa sababu wewe hujapitia huwezi kuyajua.

Wakili Safari: Hivi vipimo vyako ulikuwa unatumia nini kupima distance (umbali)?

Shahidi: Nilitumia vipimo vya meta.

Wakili Safari: Ni nani alikuwa anakushikia hiyo meta?

Shahidi: Siwezi kukumbuka tulikuwa timu kubwa.

Wakili Safari: Kuna kitu kinaitwa seizure (kukamata). Katika utaalamu wenu nini maana yake?

Shahidi: Ni fomu unayojaza vitu ulivyovichukua kwa mtu.

Wakili Safari: Seizure kama seizure unaifahamu?

Shahidi: Hilo ni neno la Kiingereza liweke kwa Kiswahili tuelewane. Mimi nafahamu seizure certificate.

Wakili Mwandamizi wa Serikali anayeendesha kesi hiyo, Abdalah Chavula alisimama na kumuomba jaji kuwa wakili aulize kwa lugha ya Kiswahili ambayo shahidi na wazee wa baraza wanaielewa vizuri.

Hata hivyo, kabla ya jaji hajatoa mwongozo, wakili Safari aliamua kuachana na hilo swali.

Wakili Safari: Wewe una elimu gani?

Shahidi: Kidato cha sita nilimaliza 1994.

Wakili Safari: Ulikuwa unasomea masomo gani?

Shahidi: Sanaa yaani Arts.

Wakili Safari: Katika taalumu ya Jeshi la Polisi, una taaluma gani?

Shahidi: Nina cheti cha upelelezi, cheti cha crime scene management, fraud investigation, counter terrorism na disaster management.

Wakili Safari: Unaweza kutuambia kozi hizo ulikuwa awarded nini?

Shahidi: Kila kozi nilipata cheti.

Wakili Safari: Kuna certificate of attendance (kushiriki) na ya ku graduate (kuhitimu), wewe ulipata nini?

Shahidi: Certificate of attendance (cheti cha kushiriki).

Wakili Safari: Lugha za kufundishia ilikuwa nini?

Shahidi: Ilikuwa Kiingereza

Wakili Safari: Sasa inakuwaje hujui neno seizure au unaidanganya Mahakama?

Shahidi: Nilikuwa sidanganyi

Wakili Safari: Wakati unafika Bomang’ombe, mwili wa marehemu ulikuwa wapi?

Shahidi: Ulikuwa umeshapelekwa mochwari.

Wakili Safari: Ieleze Mahakama hii, marehemu alivuliwa nguo zake wapi?

Shahidi: Wakati marehemu akivuliwa nguo sikuwepo.

Wakili Safari: Risasi inavyopigwa huwa inatoboa nguo?

Shahidi: Ndiyo

Wakili Safari: Ulipata ushahidi wowote wa mtu aliyekabidhiwa nguo za marehemu?

Shahidi: Sijapata

Awali Wakili Ndusyepo naye alimhoji shahidi huyo kuhusiana na ramani hiyo na baadaye kumdodosa kuhusu taratibu za makabidhiano ya vielelezo kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine.

Wakili Ndusyepo: Utakubaliana na mimi kuwa huo utaratibu wa utunzaji na makabidhiano ya vielelezo unayafanya kwa kutumia PGO (Police General Orders-Muongozo wa polisi).

Shahidi: Sina uhakika na hiyo PGO unayoisema.

Wakili Ndusyepo: Mimi nakukumbusha hiyo PGO, kwa hiyo ni kweli unafuata PGO)

Shahidi: Ndio nafuata PGO, lakini sina uhakika na hiyo PGO 229 mpaka nijikumbushe.

Wakili Ndusyepo: PGO 229 inahusu makabidhiano na handling (usimamizi) ya vielelezo. Mimi ni Ofisa wa Mahakama, huniamini?

Shahidi: Sijaisoma ila inaweza kuwa kweli.

Wakili Ndusyepo: OC-CID (mkuu wa upelelezi wilaya) ni mtu wa aina gani?

Shahidi: Ni mkuu wa upelelezi wa wilaya.

Wakili Ndusyepo: Je, wewe unaweza kuwa OC-CID?

Shahidi: Ninaweza

Wakili Ndusyepo: Unazo sifa za kuwa OC-CID?

Shahidi: Nikipendekezwa na wakubwa wangu naweza kuwa.

Wakili Ndusyepo: Je, ni kweli moja ya sifa ni kuwa mkomavu katika masuala ya upelelezi kama wewe?

Shahidi: Ndio

Wakili Ndusyepo: Sasa iambie Mahakama, kila OC-CID ni mkomavu kama wewe katika upelelezi?

Shahidi: Siwezi kusema hivyo kwa sababu siwafahamu ma OC-CID wote.

Wakili Ndusyepo: Unamfahamu mtu anaitwa Joashi Yohana?

Shahidi: Ndio namfahamu

Wakili Ndusyepo: Ni nani?

Shahidi: Alikuwa OC-CID wilaya ya Hai.

Wakili Ndusyepo: Je, mwezi Agosti, 2013 alikuwepo wilaya ya Hai?

Shahidi: Ndio

Wakili Ndusyepo: Unafahamu huyo mtu alikuwa kutoa ushahidi hapa kama PW1 (shahidi wa kwanza wa mashtaka).

Shahidi: Sina uhakika, lakini nilisikia.

Wakili Ndusyepo: Isaidie Mahakama, kati yako wewe na yeye ni nani alikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio tarehe 7.8.2013?

Shahidi: Yeye ndio alianza kufika

Wakili Ndusyepo: Nyie wapelelezi mnasema mkifika eneo la tukio mnalizuia lisiingiliwe, kwa kuwa wewe ulimkuta PW1, tumuamini nani kati yake na yeye alikuta eneo halijawa disturbed (kuvurugwa).

Shahidi: Yeyote anaweza kukuta eneo halijaingiliwa.

Wakili Ndusyepo: OC-CID alisema kwamba kielelezo namba saba yaani Pistol (bastola) na magazini alizikuta kwenye brief case nyeusi, lakini wewe umeiambia Mahakama ulivikuta mwilini mwa marehemu. Yupi anasema ukweli kati yako na OC-CID?

Shahidi: Siwezi kusema ushahidi wa mtu mwingine maana sikuusikia.

Chanzo: Habarileo