Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji wivu wa mapenzi yaongezeka

Wapenziiiii Ed Mauaji wivu wa mapenzi yaongezeka

Sat, 10 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, alisema mienendo ya hivi karibuni inaonyesha kwamba matukio ya wanawake kuuawa na wenza wao, yameongezeka kutokana na wivu wa mapenzi.

Henga alisema LHRC ilibaini kuwa mauji hayo baadhi hufanywa na wenza wanaoishi pamoja au wenza walioachana.

“Kwa mwaka 2019, LHRC ilikusanya matukio 12 ya mauaji ya wanawake yaliyofanywa na wenza wao, huku matukio manane yakihusishwa na wivu wa kimapenzi.

“Mwaka 2020, LHRC ilikusanya matukio 32 ya mauaji ya wanawake yaliyofanywa na wenza wao, matukio 23 yalisababishwa na wivu wa mapenzi. Mauaji haya ni ukatili dhidi ya wanawake na yanakiuka uhuru wao dhidi ya ukatili pamoja na haki ya kuishi,” alisema Henga na kuongeza;

“Matukio hayo ni zaidi ya mara mbili yaliyotokea mwaka 2020, ikilinganishwa yaliyoripotiwa mwaka 2019.”

Alisema haki tano kati ya zilizofanyiwa utafiti ilibainika kukiukwa zaidi ikiwamo haki ya kuishi ambayo yalihusisha mauaji yaliyotokana na watu kujichukulia sheria mkononi, imani za kishirikina na kijinsia.

Alisema haki nyingine iliyokiukwa ni haki ya uhuru wa kujieleza, utungaji na marekebisho ya utekelezaji wa sheria na ukatili wa kingono na kimwili dhidi ya wanawake, watoto na wazee.

“Ukamataji na uwekaji kizuizini watu kinyume na sheria, uchunguzi kuchelewa kukamilika, kutotoa dhamana, ubambikaji wa kesi, kukosa uhuru wa kujumuika ni kati ya haki zilizokiukwa,” alisema Henga.

Aidha ripoti hiyo ilisema kutoandaliwa kwa wosia mapema, ni kati ya sababu za chanzo cha migogoro ya ardhi huku wanawake na watoto wakiathiriwa zaidi.

“Watanzania wengi bado wana hofu ya kuandaa wosia, wakidhani wanajichulia kifo, matukio na matatizo mengi ambayo LHRC tunakutana nayo ni pamoja na masuala ya umiliki wa ardhi,” alisema Henga.

Kadhalika, ripoti ilionyesha kulikuwa na mauaji ya watu 122 yaliyotokana na imani za kishirikina pamoja na upungufu wa asilimia 42 wa watumishi katika mhimili wa Mahakama.

Alisema kama ilivyokuwa kwa mwaka 2019, idadi ya ajali za barabarani na vifo vimepungua kwa mwaka jana, kutokana na juhudi za Jeshi la Polisi na wadau.

Ripoti ilieleza kwamba ajali 10,297 zilizotokea mwaka 2016 zilipungua na kufikia 2,924 mwaka 2019, sawa na punguzo la asilimia 56 huku mwaka jana ziliripotiwa ajali 1,714 na vifo ni 1,260.

Chanzo: ippmedia.com