Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji dada Bilionea Msuya, gari linalohusishwa lapelekwa mahakamani

Msuya Dada 0 Mauaji dada Bilionea Msuya, gari linalohusishwa lapelekwa mahakamani

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: Ippmedia

Mahakama Kuu Kanda ya imepokea kielelezo cha gari aina ya Landrover lenye namba za usajili T 429 BYY kinachohusishwa katika mauji ya mdogo wa marehemu Erasto Msuya, maarufu Bilionea Msuya, Aneth Msuya, baada ya gari hilo kuhifadhiwa kwa zaidi ya miaka sita katika Kituo cha Polisi Chang'ombe.

Washitakiwa katika kesi hiyo ya mauji ni aliyekuwa mke wa bilionea huyo, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyela (40). Aneth aliuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa shingoni nyumbani kwake Kibada, Kigamboni mkoani Dar es Salaam. Uamuzi huo umetolewa na Jaji Edwin Kakolaki wa mahakama hiyo baada ya kupitilia mbali pingamizi la awali lililotolewa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala kwa madai kuwa gari hilo halikuwapo kwenye orodha ya vielelezo ambavyo washtakiwa walisomewa awali.

Jaji Kakolaki alisema kwa kutafakari maelezo ya pande zote mbili, sheria na kesi iliyohusika, mahakama inaona kuwa katika mambo mengi yaliyotajwa hayabishaniwi kuwa kielelezo kilichokusudiwa kutolewa Mahakama Kuu, lazima kiwe kimesomwa katika mahakama ya chini.

Alidai kuwa madhumuni ya kukiweka katika orodha kielelezo ni ili washtakiwa wawe na ufahamu kujua ushahidi ambao utakuwa mbele yao, basi pale panapokuwapo na kusahaulika kwa kielelezo, mhusika anatakiwa kuthibitisha katika kifungu namba 289(1)(4) cha CPA.

"Katika shauri hili, hakuna ubishi kwamba Kibatala alipewa taarifa ya kuongezwa kwa kielelezo hicho na mahakama pia. Kwa hiyo, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha taarifa hiyo kwa kufuata sheria. Kwa hiyo, kielelezo hicho kinaweza kupokewa na mahakama," alisema.

Aliongeza kuwa hadi mahakama inafikia hatua hiyo, iliona taarifa iliyotolewa na upande wa mashitaka ilikidhi vigezo vya kisheria vya kuongeza kielelezo hicho.

Baada ya uamuzi huo, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha mwaka 2016, George Katabazi aliiomba mahakama ipokee gari hilo kama kielelezo wakati akitoa ushahidi wake jinsi alivyokamata gari hilo mkoani humo na kulileta Dar es Salaam kwa ajili ya upelelezi.

Katika pingamizi hilo, Kibatala alidai kuwa kielelezo hicho hakikuwapo wakati washtakiwa wanasomewa maelezo ya mashahidi na pia hajawahi kupewa taarifa na upande wa mashtaka kuwa wanataka kuongeza kielelezo hicho na wala mahakama haina taarifa hiyo.

Alidai katika shauri namba 523/2020 dhidi ya Saidi Malikita na Jamhuri, majaji wametoa masharti ya jinsi taarifa kama hiyo inatakiwa kutolewa chini ya kifungu namba 246(2) cha CPA Sura ya 20 kama iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Marietta Maguta, alidai kuwa walimpa taarifa Kibatala kuwa wanataka kuongeza kielelezo, lakini alikataa kupokea kwa madai kuwa hatokuwa na pingamizi, lakini baada ya Jaji kumbana, alikubali kupewa taarifa hiyo.

Katika maelezo ya onyo, Miriam anaeleza kuwa aliamua kumuua wifi yake kwa sababu alikuwa 'anamfuatafuata' katika suala la usimamizi wa mirathi ya mumewe, marehemu Bilionea Msuya na katika kutekeleza mauaji hayo, alimkodi mtu ambaye alimlipa Sh. milioni 20.

Maelezo hayo ya Miriam yalisomwa mahakamani hapo na shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, WP Sajenti Mwajuma, aliyemhoji mshtakiwa huyo na kuandika maelezo yake alipotiwa mbaroni, baada ya maelezo hayo kupokewa mahakamani hapo kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Chanzo: Ippmedia