Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi dawa za kulevya yalitesa Jeshi la Polisi Tanga

Dawaaa Matumizi dawa za kulevya yalitesa Jeshi la Polisi Tanga

Mon, 11 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limesema linatafuta mwarobaini wa tatizo la uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kwa wakazi wa mkoa huo.

Pia, limesema linatamani kuona mkoa huo ukiondoka katika orodha ya vinara wa kitaifa wa matumizi ya dawa za kulevya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leopord Fungu, aliyasema hayo juzi na kueleza kuwa jeshi hilo limeanza kupata ushirikiano mkubwa wa watoa taarifa wanaowataja wauzaji wa dawa hizo pamoja na watumiaji wake.

Akizungumza na wadau mbalimbali wakati akihitimisha kampeni ya uelimishaji iliyoandaliwa na Taasisi ya Casa Familia Rosseta, Kamanda Fungu alisema: “Sisi tutawasitiri watoa taarifa, ninyi wananchi wa Tanga leteni taarifa zao.

“Tunataka kupambana kikweli kweli na dawa za kulevya na kwa mkoa wa naambiwa Casa Familia Rosseta imeshafanya midahalo mbalimbali katika shule 38 za sekondari za Tanga Jiji na Wilaya ya Muheza. Hongereni sana kwa hilo.”

Aidha, Kamanda Fungu alisema ni jambo la aibu kuendelea kuona Mkoa wa Tanga ukishika nafasi ya pili kitaifa, nyuma ya Mkoa wa Dar es Salaam katika matumizi ya dawa za kulevya.

"Katika maeneo yetu tunawajua kabisa ni nani wanaojihusisha na biashara hii tuleteeni majina kisirisiri tuna polisi kata wetu tuna polisi tarafa wetu, lakini hata mkiamuamua njooni katika ofisi zetu kutupa majina ya wahusika kisirisiri tutadili nao kwani mkitusaidia hilo Taifa letu takatifu na pendwa litakuwa na watu makini watenda kazi na wanaoitumikia vyema, "alisisitiza Fungu.

Vilevile, alisema kuwa utumiaji wa dawa hizo, unaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa watalii kutokuja nchini, huku akiahidi Kikosi cha Usalama Barabarani kuwashughulikia madereva wanaoendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia vilevi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Casa Familia Rosseta, inayojihusisha na kulea watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu, Irene Kaoneka, alisema Tanzania ni moja kati ya nchi nyingi zilizoathiriwa na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema matumizi ya dawa za kulevya, huathiri afya za Watanzania kwa kiwango kikubwa, kwa kuwa athari hizo huanzia katika ubongo.

Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi huyo alisema wamelazimika kutoa mchango wao katika mapambano hayo ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu kwa jamii kama shule za sekondari, maeneo ambayo dawa dawa za kulevya zinatumika kwa wingi na katika maeneo ya ibada ikiwamo msikitini na kanisani ili viongozi na waumini wafahamu tatizo na kutoa msaada kwa waratibu kufika katika vituo vya tiba.

Awali, Ofisa Elimu Sekondari wa Jiji la Tanga, Lusajo Gwakisa, akizungumza katika mkutano huo, aliwataka wanafunzi waliopata elimu hiyo kwenda kuisambaza vizuri na ikaweze kuleta mtazamo chanya kwa Taifa.

"Mkoa wetu kuwa wa tatu kutoka chini kielimu unachangiwa na mambo mengi sana ikiwamo watoto kuanza kutumia dawa za kulevya wakiwa na umri mdogo. Niwaase tu tukae mabalozi wazuri wa kupinga matumzi haya ya dawa za kulevya," amesisitiza Gwakisa.

Shule 38 zimefanikiwa kushiriki katika kampeni hiyo ya mapambano ya dawa za kulevya, ambapo shule 22 ziko katika Jiji la Tanga na Shule 16 ziko Wilaya ya Muheza.

Chanzo: ippmedia.com