Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matukio yaliyotikisa mahakamani mwaka 2021

Matukioa Mahakama Matukio yaliyotikisa mahakamani mwaka 2021

Wed, 29 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kesi zikiwamo za mirathi ya marehemu Reginald Mengi, wakili maarufu wa kujitegemea, Fatma Karume na ya Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Kimataifa, Bernard Membe dhidi ya mwanahabari Cyprian Musiba, ni baadhi ya kesi kubwa au maarufu zilizotolewa hukumu mwaka 2021.

Hizi ni baadhi ya kesi ambazo hukumu zake zimeacha kumbukumbu si tu kutokana na umaarufu wa wahusika, bali pia kutokana na mvutano kati ya pande mbili husika.

Kesi wosia wa Mengi

Hii ni kesi inayohusu mirathi ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini Reginald Mengi, aliyefariki dunia Mei 2, 2019, Dubai. Iliibua mvutano mkali wa mirathi yake baina ya makundi matatu tofauti nje ya mahakama na kisha mahakamani.

Makundi hayo ni familia zake mbili yaani, watoto wake wakubwa aliowazaa na mke wake mkubwa (marehemu pia) pamoja na baadhi ya ndugu zake kwa upande mmoja na mjane wake, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake wawili kwa upande mwingine.

Advertisement Kundi la tatu ni baadhi ya ndugu zake na watu wake waliodai kupendekezwa na marehemu katika wosia wake kuwa wasimamizi wa mirathi yake.

Mvutano huo ulianza baada ya kufunguliwa kwa shauri la mirathi namba 39 la mwaka 2019, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lililofunguliwa na Benson Benjamini Mengi, William Onesmo Mushi, Zoebu Hassuji na Sylvia Novatus Mushi, wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi mirathi hiyo kwa mujibu wa wosia huo.

Hata hivyo, mtoto wa marehemu, Abdiel Mengi na ndugu wa marehemu Benjamini Mengi, waliweka pingamizi dhidi ya wosia huo, wakipinga uhalali wake huku wakiwasilisha jumla ya sababu nne za kuupinga.

Sababu hizo ni pamoja na kwamba haukuwa umepigwa muhuri na saini iliyokuwepo ilikuwa ni tofauti na saini ya kawaida ya marehemu Mengi na kwamba haukushuhudiwa na ndugu au mke wa marehemu.

Pia walikuwa wakidai kuwa marehemu hakuwa na uwezo wa kuandaa wosia kwa kuwa alikuwa na matatizo ya kiafya tangu mwaka 2016, na kwamba unaondoa katika urithi watoto bila kuzingatia mila za Kichaga au kuhusisha ndugu.

Mjane wa marehemu, Jacqueline akiwawakilisha watoto wake wawili aliozaa na Mengi, naye aliwasilisha maombi kuingia kwenye shauri hilo lakini juhudi zake hazikuzaa matunda mara mbili zote, kwani maombi yake yalikataliwa kwa sababu za kisheria.

Hukumu

Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za pande zote, katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Yose Mlyambina Mei 18, 2021, ilikukubaliana na hoja za pingamizi lililowekwa na mmoja wa watoto wakubwa wa marehemu pamoja na ndugu yake marehemu, waliokuwa wakipinga uhalali wa wosia huo.

Hivyo mahakama hiyo iliukataa wosia huo uliokuwa ukidaiwa kuandikwa na marehemu Mangi pamoja na mambo mengine, ikieleza kuwa haukidhi matakwa ya kisheria ili kuwa wosia halali.

Katika hukumu hiyo Jaji Mlyambina pamoja na mambo mengine, alisema kuwa unawanyima urithi wanawe bila kutoa sababu, na kwamba ziliiingizwa mali za mke wake mkubwa na pia kwamba nakala yake alikuwa nayo mke mdogo Jacquiline Mengi ambaye alikuwa mnufaika.

Hivyo hakuwateua waombaji hao kuwa wasimamizi wa mirathi na badala yake aliwateua Abdiel na Benjamini kuwa wasimamizi wa mirathi na akaelekeza mali za marehemu zigawiwe kwa warithi wanaostahili kwa utaratibu wa kawaida kama wa mtu ambaye hakuacha wosia.

Mjane apinga hukumu

Hata hivyo, mjane wa marehemu Mengi, Jacqueline alifungua maombi ya mapitio ya hukumu hiyo iliyobatilisha wosia huo akiiomba Mahakama ya Rufani ifanye mapitio ya hukumu hiyo na hatimaye ibadilishe.

Kufuatia maombi hayo wajibu maombi wa kwanza Abdiel Reginald Mengi, na Benjamin Abraham Mengi (mdogo wake na marehemu Mengi) walimwekea Jacqueline pingamizi la awali la hoja za kisheria wakiiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali maombi yake bila kuyasikiliza.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake ilitupilia mbali hoja zote za pingamizi, badala yake ilikubali kuyasikiliza maombi hayo ya mapitio ya mjane huyo. Kwa sasa maomb yake hayo yanasubiri kupangiwa tarehe ya usikilizwaji Mahakama ya Rufani.

Kesi ya uwakili wa Fatma Karume

Hii ni kesi nyingine iliyoibua mvuatano mkali wa kisheria mahakamani baada ya wakili maarufu nchini, Fatma Aman Abeid Karume kuondolewa katika orodha ya mawakili Tanzania Bara. Kufuatia sakata hilo kwa mwaka huu wa 2021, Mahakama Kuu imetoa hukumu mbili ambazo zote zimemnufaisha mwanasheria huyo.

Karume, maarufu kama Shangazi, aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (TLS), alipewa adhabu hiyo ya kufutwa katika orodha ya mawakili Septemba 23, 2020, na Kamati ya Mawakili baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya taaluma hiyo.

Kamati hiyo ya mawakili ilifikia uamuzi huo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakati akiwasilisha hoja zake za maandishi katika kesi ya kikatiba aliyokuwa akiisimamia, iliyokuwa ikisikilizwa na aliyekuwa Jaji Kiongozi, Dk Eliezer Felesh.

Hukumu ya Membe dhidi ya Cyprian Musiba

Hii ni hukumu ya kesi ya madai ya kashfa iliyofunguliwa na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe dhidi ya mwanahabari anayejitambulisha kama mwanaharakati huru, Cyprian Musiba.

Membe alikuwa akimlalamikia Musiba kuwa alimkashfu kwa kauli zake dhidi yake katika magazeti yake ya Tanzanite katika matoleo mbalimbali na katika mitandao ya kijamii.

Oktoba 28, 2021 Mahakama Kuu katika hukumu iliyotolewa na Jaji Joaquine De Melo, ilimwamuru mwanahabari huyo kumlipa Membe jumla ya Sh6 bilioni, baada ya kukubaliana na hoja za Membe.

Hukumu ya Mattaka na wenzake

Hii ni kesi iliyokuwa ikimkabili mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Ndege nchini (ATCL) David Mattaka na na wenzake wawili; aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Ramadhan Mlinga na mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.

Walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 16, 2016 wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya ofisi, kughushi na kuisababishia hasara Serikali kupitia kutokana na mchakato wa ukodishaji wa ndege.

Mashtaka hayo yalikuwa matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya ofisi, na makosa mawili ya kuisabishia Serikali hasara ya jumla ya Dola za Marekani 42,459,316.12 zaidi ya Sh.98.3 bilioni kwa Mattaka, kughushi kwa Mlinga na Soka,

Agosti 20, mahakama hiyo iliwatia hatiani, huku Mattaka akitiwa hatiani katika mashtaka manne.

Hivyo alihukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh8 milioni (Sh2 milioni kwa kila shtaka) au kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mine.

Mlinga na Soka walitiwa hatiani katika shtaka moja la kughushi nyaraka ambapo walihukumiwa adhabu ya kulipa faini ya Sh2 milioni kila mmoja au kifungo cha mwaka mmoja jela. Wote walifanikiwa kulipa faini hiyo.

Shamimu Mwasha na mumewe

Hawa ni wanandoa, mfanyabiashara Abdul Nsembo na mkewe, Shamimu Mwasha, anayemiliki blog ya 8020 waliohukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya, aina ya aina ya heroini gramu 439.70.

Walikutwa na dawa hizo, Mei Mosi 2019, eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na walihukumiwa adhabu hiyo, Machi 31,2021.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz