Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matukio ya utekaji watoto Tanzania yawaibua wadau

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo la Ekama linalojihusisha na utetezi wa haki za watoto na wanawake limetoa wito kwa Serikali kuimarisha ulinzi katika jamii ili kudhibiti matukio mbalimbali yanayojitokeza ikiwamo watoto kutekwa.

Pia limewataka wazazi kuwa makini na watoto na kutowaruhusu kwenda maeneo ya mbali hasa katika kipindi hiki  ambacho matukio ya watoto kuibwa yameshamiri.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa watoto watano walioshiriki mdahalo uliofanyika ‘Siku ya Mtoto Duniani’, Meneja Rasilimali wa Ekama, Judith Malisa alisema ukatili wa aina hiyo haufai kufumbiwa macho na endapo hautadhibitiwa utaathiri jamii.

Alisema lengo la mdahalo huo ni kuwajengea uwezo wanafunzi waweze kujitetea, kujisimamia, kutetea haki zao na kupinga ukatili dhidi yao.

"Sisi tunaishauri Serikali kuongeza ulinzi kupitia Jeshi la Polisi ili watoto waweze kuwa salama, lakini pia tunawasisitiza wazazi wawalinde watoto," alisema.

Shirika hilo linaloendesha mradi wa ulinzi wa mtoto shuleni, linahusisha wazazi, walimu na viongozi wa Serikali za mitaa kwa kuwajengea uwezo wa namna ya kuchukua hatua pindi mtoto anapofanyiwa ukatili na jinsi ya kumlinda.

Alisema shirika hilo limefanya utafiti mwaka 2015 na kugundua kuna mazingira magumu ambayo watoto wanapitia ikiwamo kufanyiwa ukatili.

"Katika tafiti zetu tumebaini kuwa katika jiji la Dar es Salaam wilaya inayoongoza kwa watoto kufanyiwa ukatili ni Temeke hivyo hatua za makusudi za kuimarisha ulinzi zinahitajika," alisema.

Akizungumza mara baada ya kupokea cheti cha ushiriki, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Tandika, Jesca Malilo alisema kupitia mdahalo huo wamejifunza namna ya kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili.

"Mara nyingi sisi watoto tunafanyiwa sana ukatili haya yanayoendelea sasa katika vyombo vya habari kuhusu watoto kutekwa hii inaonyesha kuwa tupo katika wakati mgumu," alisema.

Jesca ameshauri watoto wenzake kuwa walinzi wa watoto wengine. "Tunatakiwa sisi wenyewe tukiona mwenzetu anafanyiwa ukatili tuwe wa kwanza kutoa taarifa tusisubiri hadi mwenzetu apate madhara," alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz