Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matukio ya utekaji na athari kwenye uwekezaji

22259 Kutekana+pic TanzaniaWeb

Sun, 14 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya tajiri namba moja Afrika Mashariki na Kati, Mohammed Dewji ‘Mo’ kutekwa, wadau wa biashara na uwekezaji wamesema endapo hatapatikana mapema huenda hali ya usalama ikawakatisha tamaa wawekezaji hasa wa nje kuja nchini.

Hilo linatokana na msemo wa Kiswahili kwamba ndege wanaofanana huruka pamoja, kwamba bilionea mmoja ana uwezo wa kuwashawishi wenzake kutokana na sifa nzuri atakazozitoa.

“Tusipoidhibiti hali hii ya utekaji, tutakuwa tunatengeneza ajira nyingine ambayo itakuwa na madhara makubwa kwa Taifa. Huko mbele, unaweza ukakuta mtu ameishiwa hela ya kula akaamua kwenda shuleni, akamkamata mtoto mmoja na kudai hela kwa wazazi wake. Tusifike huko,” alisema Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Zanzibar.

Alisema suala hilo linapaswa kukemewa na jamii badala ya kuachwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pekee ili kutoichafua picha nzuri ya Tanzania iliyojengwa muda mrefu.

Alitoa rai kwa viongozi wa dini, shule na vyombo vya habari kusaidia kuhamasisha usalama wa jamii kwa kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.

“Utekaji ni suala lililozoweleka kwenye mataifa yaliyozoea vita ambako silaha zimezagaa, si Tanzania,” alisema Profesa Semboja.

Gazeti la Forbes linamkadiria Mo kuwa na utajiri wa Dola 1.5 bilioni (Sh3.4 trilioni) na kumfanya kuwa bilionea kijana zaidi Afrika miongoni mwa mabilionea 23 waliopo barani humu mwaka huu, huku akishika nafasi ya 17 Afrika.

Kati ya mabilionea 2,208 waliopo duniani sasa, jarida hilo linamuweka Mo katika nafasi ya 1,561.

“Ingawa hatujajua sababu za kutekwa kwake, lakini kutawapa wasiwasi wawekezaji juu ya usalama wao,” alisema Profesa Samwel Wangwe, mchumi na mtafiti mwandamizi wa Repoa.

Mtaalamu wa miamba na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Profesa Evelyn Mbede alisema matukio kadhaa ya utekaji ambayo wananchi walikuwa wanayasikia yalikuwa yanahusisha imani za kishirikina, lakini mambo yanakwenda yakibadilika.

Licha ya suala hilo kuwagusa wawekezaji wengine, alisema bado linaathiri uchumi kwa sababu Mo ni mfanyabiashara mkubwa nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz