Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mattaka, wenzake ATCL wana kesi ya kujibu

49398 MATAKA+PIC

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), David Mattaka na wenzake wawili, wataanza kujitetea April 10, mwaka huu, baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.

Hatua hiyo inatokana na washtakiwa hao kukutwa na kesi ya kujibu, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wa mashahidi 18 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mbali na Mattaka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk Ramadhan Mlinga na aliyekuwa mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh71 bilioni, linalomkabili Mattaka.

Wakili wa Serikali, Faraji Nguka amedai leo Ijumaa Machi 29, 2019 kuwa shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe kwa ajili ya washtakiwa hao kuanza kujitetea.

Nguka baada ya kueleza hayo, Hakimu Augustina Mmbando, aliahirisha kesi hiyo hadi April 10, mwaka huu ambapo washtakiwa hao wataanza kujitetea.

Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi katika kesi hiyo, ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo Paul Kimiti (73) ambaye alidai kuwa aliamua kujiuzulu wadhifa wake wa ujumbe wa bodi wa ATCL, baada ya kubaini kuwa menejimenti ya shirika hilo, ilikuwa inakodi ndege bila kufuata utaratibu.

Alidai menejimenti ya ATCL ilifanya uamuzi mbaya wa kukodi ndege bila kuishirikisha bodi, jambo lililosababisha hasara kwa Serikali.

Katika ushahidi, Kimiti alidai kuwa aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya ATCL, mwaka 2007, lakini ilipofika mwaka 2009, aliamua kujiuzulu nafasi yake, kutokana na menejiment ya ATCL kukodi ndege aina ya Airbus 320-214 kutoka kampuni ya Wallis Treding, bila kuishirikisha bodi ya ATCL.

Shahidi mwingine ni Julieth Matechi (48) kutoka Takukuru, ambaye alisema kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk. Ramadhan Mlinga na mwanasheria wa mamlaka hiyo Bertha Soka, walighushi muhtasari wa kikao, wakionyesha kuwa mamlaka hiyo imeidhinisha ATCL kukodi ndege.

Matechi alidai kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA zilizopo wilaya ya Ilala, Dk Mlinga na Soka, walighushi muhtasari wa  kikao wa tarehe hiyo, wakionyesha kwamba PPRA, ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL kukodisha ndegi.,

Akitoa ushahidi wake, Matechi alidai kuwa muhtasari huo wa kikao ulioghushiwa, ulionyesha kuwa mjumbe wa kikao hicho ni Mlinga huku Soka akiwa katibu.

Alidai kuwa wajumbe waliorodheshwa katika kikao hicho ni Hezra Musa na Amini Mcharo, kutoka  wizara ya fedha, wakati washtakiwa hao wakijua kuwa wajumbe hao hawakuwahi kuhudhuria kikao hicho kwa sababu walikuwa nje ya mkoa wa Dar es Salaam, kikazi.

“Baada ya kupata muhtasri wa kikao hicho, tuliwahoji wajumbe wa kikao hicho ili kujiridhisha kama kweli walishiriki katika kikao hicho au laa,” alidai Matechi.

Shahidi huyo alidai kuwa walianza kwa kumhoji, Hezra ambaye alikana kushiriki kikao cha Machi 19, 2008 kwa maelezo kuwa aliondoka nchini Machi 17, 2008 kwenda Uingereza kikazi na alirudi nchini April 4, 2008.

Kwa upande wa Mcharo naye alikana kuhusika na kikao hicho kwani Machi 17, 2008 aliondoka Dar es Salaam kwenda mkoani Manyara kikazi na alirudi jijini Machi 21, 2008.

Alibainisha kuwa baada ya kupata maelezo ya wajumbe hao, walipata nyaraka kutoka Wizara ya Fedha zilizoonyesha kuwa wajumbe hao hawakuwepo katika kikao hicho kilichofanyika Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA zilizopo wilaya ya Ilala.

“Baada ya kufanya uchunguzi wetu, tulibaini kuwa kikao hicho hakikufanyika na maelezo yaliyopo katika  muhtasari wa kikao hicho ni ya uongo na muhtasari huo ni wa kughushi kinyume cha sheria na hivyo uchunguzi wetu ulipelekea Soka na Mlinga kuwa watuhumiwa,” alidai shahidi huyo.

Katika kesi ya msingi, Mattaka, inadaiwa kuwa Oktoba 9, mwaka 2007, wakati akitekeleza majukumu yake kama Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus na kwamba mkataba huo unadaiwa  kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh71 bilioni.

Katika shtaka la kughushi linawakabili Dk Mlinga na Soka, inadawa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA zilizopo wilaya ya Ilala, washtakiwa  walighushi muhtasari wa kikao wa tarehe hiyo, wakionyesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL kukodisha ndege, wakati wakijua kuwa ni uongo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz