Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matapeli 15 kwa njia ya sms sasa mikononi mwa polisi

Fri, 29 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu 15 kwa kujihusisha na wizi kwa njia ya mtandao.

Akizungumza jana, kaimu kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Liberatus Sabas alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya msako uliofanyika kwa siku saba.

Alisema walifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali ambao wamekuwa wakipokea ujumbe mfupi wa maneno ukiwashawishi kutuma fedha kwenye namba nyingine.

“Jeshi la Polisi lilifikia hatua hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 15, baadhi yao wamekamatwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Sabas.

Alisema kuanzia Aprili 2018 kumekuwa na ujumbe mfupi wa maneno ambao umekuwa ukitumwa kwa watu mbalimbali wenye maneno, “Nitumie hiyo hela katika namba hii namba ile ya awali ina matatizo nitumie sasa hivi” na mwingine unaosema, “Mganga wa jadi msamaria, je unasumbuliwa na magonjwa sugu, ndoa, pesa na majini wasiliana kwa namba 0742- 138389 huduma itakufuata ulipo.”

Sabas alisema, watuhumia wa utapeli huo pia wamekuwa wakitumia namba 0758-713746, 0764-581220 na 0744-105579 kutuma ujumbe huo mfupi.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao walikutwa na simu 45, kadi za simu 352 zikiwa na usajili tofauti pamoja na kompyuta mpakato tatu na baada ya mahojiano wamekiri kutumia mfumo wa ‘back sms’ wenye uwezo wa kutuma kwa watu 1,000 kwa wakati mmoja.

Kamanda Sabas alisema uchunguzi unaendelea na utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani.

Mwananchi liliwahi kuchapisha habari kuhusu matapeli hao iliyokuwa na kichwa cha maneno yasemayo ‘Kaa chonjo na sms zinazokuelekeza kutuma hela’

Katika habari hiyo, lilizungumza na waathirika mbalimbali wa utapeli huo pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kaimu meneja Uhusiano wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema hawana jukumu kisheria la kushughulikia uhalifu wa mitandao.

Alisema wanachofanya ni kushirikiana na kitengo cha uhalifu wa mitandao kilichoko katika Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kiteknolojia.

“Kama kuna kesi inahitaji uchunguzi wa kiteknolojia tunashirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha uhalifu wa mitandao tofauti na hapo hatuna haki wala sheria ya kushughulikia suala hilo,” alisema.

w

Chanzo: mwananchi.co.tz