Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maswali kibao mwandishi wa habari anayeshikiliwa polisi

Wed, 31 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limekiri kuwa linamshikilia mwandishi wa habari za kiuchunguzi, Erick Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake jambo ambalo limeacha maswali miongoni mwa wadau wa habari nchini.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza na wanahabari jana alisema wanamshikilia Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake na kwamba walimkamata juzi baada ya kupelekewa wito wa kutakiwa afike polisi, lakini akakaidi.

“Mwandishi huyo aliandikiwa barua ya wito kwa ajili ya mahojiano, lakini alikaidi kutii wito huo. Kila mmoja anapaswa kutii wito bila shuruti na kila mmoja anapaswa kutii ili kuondoa msuguano usiokuwa na lazima. Polisi tunapomwita kwa hiari akakaidi tunatumia mamlaka tuliyopewa kisheria,” alisema Mambosasa.

Jambo hilo limeacha maswali kutokana na juzi jioni watu wanaodaiwa kuwa polisi wakiwa wamevaa kiraia kufika nyumbani kwa Kabendera maeneo ya Mbweni na kumchukua kwa nguvu wakidaiwa kugoma kuonyesha vitambulisho.

Hii si mara ya kwanza kwa Kabendera kuhojiwa kuhusu uraia wake kwani mwaka 2013 Idara ya Uhamiaji ilimuhoji kuhusu suala hilo.

Uchunguzi huo kuhusu uraia wa Kabendera ulifanywa na kamati iliyoundwa na waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Dk Emmanuel Nchimbi.

Pia Soma

Juzi usiku Mwananchi lilipowatafuta kwa nyakati tofauti lilizungumza na kamanda wa Polisi Kinondoni, Mussa Taibu pamoja na kamanda wa polisi kanda hiyo, Lazaro Mambosasa waliosema hawana taarifa ya tukio hilo huku wakiahidi kufuatilia.

Kwa taarifa zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumatano Julai 31, 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz