Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashuhuda wasimulia ofisa wa LHRC alivyokamatwa

89446 PIC+MAGOTI Mashuhuda wasimulia ofisa wa LHRC alivyokamatwa

Sat, 21 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tito Magoti, ofisa wa kitengo cha elimu kwa umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jana asubuhi alikamatwa maeneo ya Mwenge na kuzua taharuki kwenye mitandao ya kijamii, watu wengi wakidhani ametekwa.

Hata hivyo, polisi walituliza taharuki hiyo baada ya jioni kutoa taarifa kuwa inamshikilia ofisa huyo.

Wakati taasisi mbalimbali za masuala ya haki za binadamu na baadhi ya wanasiasa wakianza kupaza sauti kutaka Magoti aliyekamatwa jana saa nne asubuhi karibu na kituo cha mafuta cha Puma, Mwenge kuachiwa popote alipo, jioni kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alitoa taarifa kuwa wanamshikilia.

Mambosasa alisema Magoti pamoja na watu wengine watatu wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano, akisisitiza kuwa hakutekwa kama ilivyokuwa ikidaiwa. “Yupo katika mikono salama na wote kwa pamoja wanaendelea kuhojiwa kwa tuhuma za makosa ya jinai. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya kukamilisha uchunguzi na mahojiano,” alisema Mambosasa.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la James ambaye ni mlinzi wa duka lililopo karibu na eneo hilo alisema, ilifika gari aina ya Toyota Harrier ya kijivu ikiwa na watu watatu na kuegeshwa eneo hili (huku akionyesha kwa kidole).”

Alisema baada ya muda alishuka mtu mmoja mrefu aliyevaa shati jeusi na kujitambulisha kuwa yeye ni askari na wanataka kumkamata mhalifu.

“Kuna mhalifu tunamfuatilia na yupo eneo hili tunahitaji kumkamata hivyo ukiona chochote usishangae,” alisema James akimnukuu askari huyo.

Mlinzi huyo alisema baada ya muda ilikuja pikipiki ikiwa na abiria mmoja na kusimama mbele ya duka hilo, “ilipofika kwenye lile gari aliteremka mtu mwingine na kumfuata yule abiria kwenye pikipiki na kumkamata akiwa amevaa kofia ngumu.”

Alisema walikuwa wakivutana na walisogea hadi kwenye gari hilo na kumfunga pingu, “walipogundua hajamlipa mwenye pikipiki walimfungua na kumtaka akamlipe. Sisi hatukushangaa kwa kuwa walitoa taarifa na mtu aliyekamatwa hakuwa anapiga kelele hivyo walimweka ndani ya gari na kuondoka naye.”

Kuhusu kuwepo kwa kamera za ulinzi CCTV eneo hilo, mlinzi huyo alieleza kuwa zimeharibika muda mrefu na bado hazijatengenezwa.

Shuhuda mwingine ambaye ni mfanyakazi wa kituo hicho cha mafuta kwa sharti la kutotajwa jina alisema “kwenye saa tano hivi asubuhi nikiwa namuhudumia mteja ghafla niliona purukushani za watu. Sikuwa na wasiwasi nilidhani wanafahamiana, ila baadaye nikasikia watu wanasema amechukuliwa na polisi na habari zikazagaa hivyo.”

Polisi wazungumza

Akimzungumzia Magoti ambaye ni mkazi wa Ubungo Kibo, Kamanda Mambosasa alisema “baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo tumesikia taarifa mbalimbali zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ametekwa, tunapenda kuutaarifu umma kuwa hajatekwa na hakuna matukio ya utekaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam na hali ya ni shwari kabisa.”

Wanasiasa, taasisi walaani

Katika taarifa yake mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga alieleza masikitiko yake kutokana na tukio hilo, “LHRC tunakemea vikali vitendo vya utekaji kwani ni mwendelezo wa ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwamo haki ya ulinzi binafsi,” alisema.

Chama cha ACT Wazalendo kupitia katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano, Ado Shaibu kilitoa taarifa na kueleza kuwa huenda Magoti amechukuliwa na polisi.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kupitia taarifa yake iliyosainiwa na mratibu wake, Onesmo Ole Ngurumwa imeeleza kusikitishwa na taarifa za kutoweka kwa mwanasheria huyo ambaye pia ni mfanyakazi wa LHRC.

“Matukio kama hayo yameendelea kushamiri hasa kwa watetezi wa haki za binadamu, tunaliomba jeshi la polisi kuchukua hatua za haraka za makusudi kuhakikisha mtetezi huyu anapatikana akiwa salama,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz