Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashuhuda wasimulia mauaji baa Dar

5b247248cdb230040e9d319656380a39 Mashuhuda wasimulia mauaji baa Dar

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MASHUHUDA wamesimulia namna mfanyabiashara, Alex Korosso alivyomuua kijana aliyetambulika kwa jina la Gift Jumamosi iliyopita.

Ilidaiwa jana kuwa Korosso siku ya tukio saa nne asubuhi alifika katika duka la kuremba magari Sinza kwa Remmy linalomilikiwa na mfanyabiashara Muddy.

Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA), Chiki Mchoma alisema jana kuwa Korosso alikuwa mhasibu wa chama hicho.

HabariLEO jana lilifika katika eneo la tukio na kukutana na Rashid Salum ambaye ndiye aliyempokea mfanyabiashara Korosso kwenye duka la kuremba magari.

Salum alisema wakati akiendelea na kazi aliyopewa na Korosso, mteja wake alienda katika baa iliyoko jirani na duka hilo iitwayo Lemax.

“Kazi hiyo tuliifanya pamoja na mwenzangu na rafiki yangu mkubwa aitwaye Zawadi Mushi maarufu kama Gifti na ilipofika saa 10:30 jioni tulikuwa tumemaliza kazi, Gifti akaenda kumjulisha kuhusu kukamilisha kazi mimi nikabaki na funguo ya gari,” alisema Salum.

Alisema baada ya muda aliamua kulisogeza gari hilo katika baa ili wasimsumbue mteja wao kwenda na kurudi.

Alisema baada ya kufika katika baa hiyo alishtushwa na milio ya risasi mfululizo hali iliyosababisha atoke haraka katika gari na kulifunga.

Alisema wakati huo Gifti alikuwa chooni na baada ya kupita dakika kama mbili za ukimya, aliamua kutoka na kukutana uso kwa uso na Korosso na kumhimiza asifanye hivyo kwa kuwa si sawa.

“Wakati Gifti akimsihi hivyo tulikuwa tunashuhudia lakini kwa kujificha, Korosso ak amuuliza kwa hiyo unataka nimfyatulie nani? Kabla Gifti hajajibu akapigwa risasi ya mguuni. Gifti alivyojua kwamba huyu sio mtu mzuri huku akitokwa na damu akajaribu kumshika,” alisema Salum.

Alisema Gifti alipigwa risasi mbili nyingine tumboni, akageuka ili kujiokoa akapigwa risasi nyingine pajani akaanguka chini.

Salum alisema kwa kuwa mtuhumiwa alikuwa amelewa na milio ya risasi ni kama imemtibua alianza kusaka watu kwenye baa hiyo na kila aliyejitokeza alifyatuliwa risasi akiwemo meneja wa baa hiyo..

Alidai kuwa baada ya mtuhumiwa kumkosa mtu mwingine alirudi kwa Gifti aliyekuwa akilalamika chini huku akimuomba asimuue lakini alipigwa risasi nyingine ya shingo na ya utosini.

Shuhuda mwingine wa tukio hilo Christopher Kigosi ambaye wakati wa tukio alikuwa akipata kinywaji alidai baada ya kumpiga risari ya kichwa Gifti, mtuhumiwa huku akiwa amesimama alijaribu kujipiga risasi ya kichwa lakini bastola yake ilikuwa imeishiwa risasi.

“Akaingiza mkono mfukoni na kutoa magazine ya risasi na kuikoki katika bastola yake, cha ajabu hakujipiga pale alipokuwa amesimama bali alisogea na kukaa katika kiti na kujifumua kichwa na kufa hapohapo. Kwa kweli ilikuwa faraja kwetu na hali ya utulivu ikarejea baada ya saa nzima ya vurugu,” alidai Kigosi.

Simulizi za watu wanaomfahamu Gifti walidai kuwa kijana huyo amekufa kwa sababu ya kazi aliyoipenda ya kutaka suluhisho la matatizo kila yanapotokea.

“Hata hapa unaweza kuona amekufa akiwa katika harakati za kuleta amani na kuokoa watu wasidhurike,” alisema jirani na Gifti, Jamal Nzunda.

Nzunda alidai kuwa haikuwa mara ya kwanza kwa Korosso kutoa bastola akiwa baa na kwamba aliwahi kufanya hivyo eneo lingine Sinza akilazimisha muziki uzimwe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz