Dar Es Salaam. Dereva teksi, Mousa Twaleb (46) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Mei 28, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kumteka nyara mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.
Mbali na shtaka la utekaji, Twaleb anakabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha Sh8milioni pamoja na kujihusisha na genge la uhalifu.
Twaleb, mkazi wa Tegeta amefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi.
Akisoma mashitaka hayo wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wankyo Simon amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 42/2019.
Kadushi amedai katika shtaka ya kwanza, mshtakiwa alijihusisha na genge la uhalifu.
Wakili Kadushi amedai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Johannesburg, Afrika Kusini, kwa makusudi alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.
Habari zinazohusiana na hii
Katika shtaka la pili, Twaleb anadaiwa Oktoba 11, 2018 katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum iliyopo wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani, walimteka nyara Mo kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.
Katika shtaka la tatu, wakili Simon amedai Julai 10, 2018 katika maeneo ya Mbezi Beach wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alitakatisha fedha Sh8milioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.
Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, Hakimu Shaidi amesema hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Wakili Kadushi amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, kwamba wanafuatilia taratibu za kisheria kwa ajili ya kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu.
Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 11, 2019 itakapotajwa.
Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa n dhamana.
Mo alitekwa nyara Oktoba 11, 2018 i katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum alikokwenda kufanya mazoezi na kupatikana Oktoba 20, 2018 katika eneo la Gymkhana.