Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashitaka kutofunguliwa hadi upelelezi ukamilike

2db369799a486865a1802a1ffffaa8c0.PNG Mashitaka kutofunguliwa hadi upelelezi ukamilike

Sat, 5 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeandaa marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kwa kuongeza kifungu kipya kinachoweka masharti ya kutofungua mashtaka mpaka upelelezi utakapokamilika, isipokuwa kwa makosa makubwa.

Marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambayo ni miongoni mwa sheria tisa katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 7 wa Mwaka 2021, kimeongezwa kifungu kipya ili kuweka masharti ya kutofungua mashtaka mpaka upelelezi utakapokamilika, isipokuwa kwa makosa makubwa.

Madhumuni ya marekebisho haya yaliyomo katika muswada huo utakaosomwa bungeni Jumatatu ijayo, ni kupunguza msongamano katika magereza na kuboresha masharti yanayohusiana na mchakato wa makubaliano ya kukiri kosa.

Marekebisho pia yanapendekeza kuongeza kifungu kipya kwa lengo la kutoa mamlaka kwa polisi kufanya operesheni za kificho kwa madhumuni ya kuzuia utendaji wa makosa.

Kwa mujibu wa muswada huo, kifungu hicho kinatoa kinga ya kutowajibishwa kwa polisi anayefanya kazi ya kificho pindi anapotenda kosa wakati wa kutekeleza majukumu yake ya operesheni za kificho.

Pia yapo marekebisho katika kifungu cha 91 kwa madhumuni ya kuzuia kukamatwa tena kwa mtuhumiwa aliyeachiwa kutokana na uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka kuondoa mashtaka kwa “nolle prosequi” kwa mujibu wa kifungu hicho cha 91, isipokuwa kama kuna ushahidi wa kutosha.

Pia vifungu vya 174, 265 na 285 vinavyoweka masharti ya kuwepo kwa Wazee wa Baraza kwenye mashauri katika Mahakama Kuu vinapendekezwa kurekebishwa au kufutwa kwa lengo la kufanya uwepo wa Wazee wa Baraza katika usikilizaji wa mashauri katika Mahakama Kuu kuwa suala la hiari.

Muswada huu pia unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, kwa kuweka kiwango kisichopungua Sh bilioni moja kwa makosa ambayo Divisheni ya Mahakama Kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi itakuwa na mamlaka ya kifedha kusikiliza.

Pia Kifungu cha 29 kinarekebishwa ili kuzipa uwezo mahakama za chini kutoa dhamana kwa makosa yenye thamani isiyopungua Sh milioni 300, lengo likiwa ni kupunguza mlundikano wa mashauri.

Muswada pia unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 ambako masharti mbalimbali katika sheria yanarekebishwa ili kuongeza kiwango cha adhabu ya faini inayoendana na hali ya uchumi uliopo kwa lengo la kuzuia utendaji wa makosa chini ya sheria.

Pia kuna mapendekezo ya kupunguza adhabu ya kifo hadi kifungo cha miaka 30 jela kwa atakayekutwa na kosa la kuchoma mali.

Kifungu cha 310 kinarekebishwa kwa kuongeza adhabu kutoka miaka saba hadi miaka 14 jela kwa watakaokutwa na kosa la kufanya mazoezi ya kijeshi (drilling) huku Kifungu cha 114(2) kikiongeza adhabu kutoka kifungo cha mwezi mmoja jela hadi miezi sita kwa atakayekutwa na kosa la kudharau mahakama.

Muswada pia unapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Veterinari kuhusu usajili wa muda kinapendekezwa kurekebishwa kwa lengo la kuwawezesha madaktari wa wanyama kutoka nchi nyingine kufanya kazi mahususi pekee, lengo likiwa ni kuhakikisha usimamizi madhubuti wa huduma zinazotolewa na madaktari wageni nchini.

Vile vile muswada huo unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori kwa lengo la kukiwezesha chuo kutoa shahada na kupanua wigo wa majukumu ya chuo ili kujumuisha utoaji wa huduma za utafiti na ushauri elekezi kwenye masuala ya utalii na nyanja zinazohusiana nayo.

Muswada huu unapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kwa lengo la kuwawezesha watu wasioona na wenye uono hafifu kuweza kupata machapisho mbalimbali katika muundo unaofikika.

Katika eneo hilo, pia kunapendekezwa kubainisha aina ya kazi zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini au kusafirishwa nje ya nchi, lengo likiwa ni kudhibiti kazi kutoka nje zisikiuke mila, desturi na utamaduni wa nchi.

Muswada pia unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa lengo la kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo. Sheria zingine zinazofanyiwa marekebisho kwenye baadhi ya vifungu ni Sheria ya Upatikanaji wa Huduma ya Mawasiliano kwa Wote, (Sura ya 422), Sheria ya Taifa ya Mashtaka, Sura ya 430.

Akiwasilisha maoni mbele ya Kamati ya Kudumu la Bunge ya Katiba na Sheria iliyoongozwa na Najima Giga, Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alipongeza serikali kwa kusudio la mabadiliko yanayolenga kuboresha mfumo wa haki jinai uliokuwa unaibua malalamiko miongoni mwa wananchi.

“Tulikuwa na tatizo la kumkamata mtu na kumfikisha mahakamani unasema upelelezi haujakamilika, sasa katika mabadiliko peleleza kwanza ndio mshitaki, hiki ni kitu kizuri, lakini sheria inasema isipokuwa kwa mashtaka yanayofikishwa Mahakama ya Rufaa, sasa sisi tunasema yawe kwa makosa ya mahakama zote,” alieleza Massawe.

“Hiki ni kitu kizuri sana maana kilikuwa kinalalamikiwa na wadau wa haki jinai, lakini pia tuseme hata kama atashitakiwa basi kuwe na muda maalumu wa upelelezi ili kutotoa fursa ya wapelelezi kupeleleza kwa muda wanaoutaka,” aliongeza ofisa huyo wa LHRC.

Alisema lingine ni kupunguzwa kwa adhabu ya makosa ya kuchoma moto mali kutoka kifungo cha maisha hadi miaka 30 ambayo ina unafuu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live