Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashine 24 za kubeti zakamatwa, zateketezwa

843c8d9d8526500f4e9c7402727d706c Mashine 24 za kubeti zakamatwa, zateketezwa

Thu, 13 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Michezo ya Kubahatisha nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Katavi, imekamata na kuziteketeza kwa moto mashine 24 za michezo ya kubahatisha zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 46.

Mashine hizo ambazo nyingine ziligundulika kuwa ni feki na baadhi zikiwa zimeingizwa nchini kinyemela bila kufuata utaratibu, zilikamatwa kwa nyakati tofauti na kuteketezwa kwa moto katika mikoa ya Katavi na Rukwa.

Katika mkoa wa Katavi, mashine nane zenye thamani ya Sh milioni 12 zilikamatwa wilayani Mlele katika mji wa Inyonga na kijiji cha Majimoto na kuteketezwa kwa moto.

Katika mkoa wa Rukwa zilikamatwa mashine 16 zenye thamani ya Sh milioni 30 katika vijiji vya mwambao kwa Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga. Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, James Mbalwe, jana alisema serikali imeweka utaratibu wa kisheria wa uingizaji wa vifaa mbalimbali kutoka nje ili iweze kunufaika kupitia ukusanyaji kodi.

Alisema mashine hizo kabla ya kuingizwa nchini, mhusika anatakiwa kupata kibali, kulipia kodi na kusajiliwa na kisha kuruhusiwa kuweka mashine kwenye eneo la biashara.

“Sekta hii imekuwa ikichangia sehemu kubwa ya mapato ya nchi yetu, kwa mwaka wa fedha 2019/20 pekee imechangia zaidi ya Sh bilioni 95 katika Pato la Taifa,” alisema.

Alieleza kuwa, kwa mujibu wa sheria, mashine hizo zinatakiwa kuwekwa katika maeneo ya kuuzia vileo, nyumba au maduka maalumu yaliyosajiliwa na waendeshaji kulipa kodi.

Meneja wa TRA mkoa wa Katavi, Matilda Kunenge, alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema, walibaini wahusika wa mashine hizo wamekwepa kulipa kodi ya serikali kwa miezi sita yenye thamani ya Sh milioni 4.2.

Naye Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa Rukwa, Chacha Boaz, alisema msako huo ni endelevu ili kuwabaini wanaokwepa kulipa kodi kwa kutumia mashine feki na zinazoingizwa nchini kinyemela bila kusajiliwa.

Chanzo: habarileo.co.tz