Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashahidi wakwamisha kesi ya aliyekuwa mhasibu wa Takukuru

20459 Mhasibu+pic TanzaniaWeb

Wed, 3 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato halali, inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na mwenzake, imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sababu mashahidi waliotakiwa kutoa ushahidi wameshindwa kufika mahakamani.

Pamoja na Gugai, washtakiwa wengine, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Wakili wa Serikali, Pius Hila akisaidia na Vitalis Peter ameeleza hayo, leo Oktoba 2, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

"Kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi, lakini mashahidi waliowategemea wameshindwa kufika Mahakamani hapa kwa sababu wapo nje ya mkoa wa Dar es Salaam," amesema

Wakili Hila amedai waliita mashahidi kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam, lakini wameshindwa kufika kwa kuwa Mtendaji wa Mahakama hakuwa na fungu la  fedha, kwa  ajili ya kuwalipa.

Soma zaidi:

·Mahakama yachachamaa kesi ya mhasibu Takukuru

 

·Kesi ya Mhasibu wa Takukuru Hakimu asema upande wa mashtaka utapata tabu sana

"Lakini  hapa tumepata  kibali kutoka kwa  Mtendaji wa Mahakama ambacho kinaelezea malipo yatasubiri fedha zitakapoingia, hivyo mashahidi wameshindwa kuja kwa  gharama zao wenyewe" amedai Hila

"Kutokana na hali hiyo, tunaomba tarehe fupi kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji" amedai Hila.

Hila baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa akisaidiana na Semi Malimi, wameutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi wengine ambao hawahitaji kuombewa kibali au hawatoki nje ya mkoa wa Dar Es Salaam ili kesi hiyo iweze kuendelea.

 

" Tuna maombi mawili, kwanza jitihada ziendelee za kuwapata mashahidi hao waliopo nje ya mkoa wa Dar es Salaam, pili; ni rai yetu kwa  mahakama walete mashahidi ambao hawahitaji kuombewa kibali na hawatoki nje ya mkoa wa Dar es salaam ili kesi hii iweze kuendelea," amedai Wakili Mgongolwa.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Hakimu Simba amesema mahakama itaongea na Mtendaji wa Mahakama ili aweze kutafuta fedha sehemu yoyote ili mashahidi hao waweze kuletwa mahakamani hapo.

"Tutaongea na mtendaji wa mahakama atafute fedha sehemu yoyote ili mashahidi waweze kuja mahakamani na kutoa ushahidi kwa sababu kesi hii ni ya muda mrefu," amesema Hakimu Simba

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi  Oktoba 15 na 16, 2018 itakapoendelea.

Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka, Ayoub Akida(52) ambaye ni Ofisa Utumishi Mkuu kutoka Takukuru, ameshatoa ushahidi wake dhidi ya Gugai.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, katika Mahakama hiyo.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh 3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa cha zaidi ya  Tsh.milioni 800,huku akishindwa kuzitolea maelezo.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz