Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashahidi wakwamisha kesi ya 'Mpemba wa Magufuli'

Thu, 23 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikiliza ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili  Yusuf Ali Yusuf maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli’.

Kesi hiyo imeshindwa kuanza kusikiliza ushahidi  leo Alhamisi Mei 23, 2019 kwa kile kilichoelezwa na upande wa mashtaka kuwa mashahidi  wameenda kwenye operesheni maalumu ya Jeshi la Polisi.

Yusuf na wenzake watano  wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Wakili wa Serikali,  Sylivia Mitato ameeleza hayo leo wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani hapo wa ajili ya ushahidi.

Mitanto amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa amepewa taarifa kuwa mashahidi waliopaswa kutoa ushahidi katika kesi hiyo wapo katika operesheni hiyo.

Kufuatia taarifa hiyo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 30, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Pia Soma

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.

 

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na mtandao wa ujangili

katika kesi ya uhujumu uchumi namba 53/2016.

 

Miongoni mwa shtaka moja kati ya mashtaka manne yanayowakabili washtakiwa hao ni  kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016, katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 180,000 sawa na Sh392,817,600 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz