Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashahidi waeleza simu za marehemu Milembe wa GGM zilivyopatikana

HUKUMU Mashahidi waeleza simu za marehemu Milembe wa GGM zilivyopatikana

Tue, 9 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Geita (GGM), Milembe Seleman imeanza kuunguruma leo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi.

Katika ushahidi wao mahakamani hapo jana Jumatatu Aprili 8, 2024, shahidi wa pili na wa tatu wameeleza namna simu za marehemu Milembe zilivyopatikana kwenye shimo la choo.

Mashahidi hao ni shahidi wa pili, H4050 Koplo Philemon, anayefanya uchunguzi wa kisayansi wa makosa ya jinai na Noel Ngasa (41) mwenyekiti wa Mtaa wa Mwatulole.

Akiongozwa na mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali, Merito Ukongoji, Koplo Philemon ameieleza Mahakama kuwa Mei 7, 2023 alipokea maelekezo kutoka kwa mkuu wa kitengo cha uchunguzi wa kisayansi, ACP Geofrey, akimtaka kwenda na mtuhumiwa eneo alilodai alitupa simu za marehemu.

Koplo Philemon ameieleza Mahakama kuwa akiwa na mshtakiwa wa tatu, Genja Deus Pastory walifika eneo la Mwatulole na mshtakiwa kuwaonyesha eneo la shimo la choo alikotumbukiza simu hizo.

Ameeleza kuwa baada ya kuona eneo hilo walilizungushia utepe, kisha wakatafuta mafundi waliolibomoa shimo hilo na kuzama kuingia wakatoa simu mbili aina ya Iphone na Sumsang.

Koplo Philemon amedai baada ya kupokea simu hizo, aliziweka kwenye vifaa maalumu na kumimina kimiminika cha kukausha na kuua bakteria, kisha kuziwasha lakini simu moja haikuwaka.

Hata hivyo, amedai kwa msaada wa ndugu wa marehemu alithibitisha kuwa simu hizo ni za ndugu yake na akajaza fomu ya upekuzi iliyoshuhudiwa na mwenyekiti wa mtaa wa Mwatulole, ndugu wa marehemu na watu wengine watatu.

Akihojiwa na wakili wa utetezi, Lebaratus John anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, aliyetaka kujua kama kuna mahali alipojaza rangi za simu alizotoa chooni, shahidi amejibu kuwa hakuna.

Wakili mwingine wa utetezi, Laurent Bugoti alitaka kujua aina ya choo zilimokutwa simu na shahidi akaeleza kuwa ni choo cha shimo cha kuchuchumaa chenye bomba, lakini alipoulizwa uhusiano uliopo kati ya mshtakiwa na mwenye choo, shahidi huyo alidai hajui.

Kwa upande wake, shahidi wa tatu, Ngasa amedai kuwa Mei 7, 2023 saa 2asubuhi alipokea simu kutoka kwa askari polisi waliomtaka kwenda eneo yalikotokea mauaji ya Milembe, kwa kuwa mtuhumiwa alikuwa anakwenda kuonyesha sehemu simu za marehemu ziliko.

Alidai kuwa saa 5 asubuhi, askari polisi wakiwa na mtuhumiwa aliyemtaja kwa jina la Genja Deus, (mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo) aliwaongoza hadi nyumbani kwa Martha Kaswahili na kumkuta mtoto wa mwenye nyumba aliyefahamika kwa jina la Anastazia Gervas.

Shahidi huyo alidai kuwa askari walimtaka mtuhumiwa kuonyesha simu zilipo na kwamba mtuhumiwa aliwaongoza hadi kwenye shimo na kuonyesha bampa la shimo la choo.

Alidai kuwa polisi walitafuta wazamiaji watatu walioingia ndani ya shimo kwa kutumia kamba na akatoka na simu mbili aina ya Iphone na Sumsang.

Ngasa alidai baada ya kutolewa simu hizo askari polisi walitoa fomu ya upekuzi na kusaini kama shahidi.

Shahidi huyo akiwa mahakamani hapo alimtambua mtuhumiwa aliyewaongoza kwenda kuonyesha alikoficha simu hizo ambaye ni Genja Deus Pastory.

Akihojiwa na wakili wa utetezi, Bugot, shahidi huyo alieleza wazamiaji hao walioingia chooni wawili walikuja na askari. huku mmoja akitoka kwenye mtaa huo wa Mwatulole.

Shahidi huyo alieleza kuwa wazamiaji hao waliingia na nguo zao, lakini walijipaka kitu kama mafuta ya taa na kwamba hawakukaguliwa kabla ya kuingia ndani ya shimo.

Wakili Erick Lutehanga anayemtetea mshtakiwa wanne, alimtaka shahidi huyo kutazama simu alizodai zimetolewa ndani ya shimo na kutaka amwambie rangi na majina.

Katika majibu yake, shahidi huyo alijibu kuwa simu ya Iphone ilikuwa nyeupe tofauti na nyeusi aliyosema awali, huku ya Sumsang ikiwa imeandikwa Tecno badala ya Sumsang kama alivyodai.

Awali, shahidi wa kwanza, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo Kijava aliieleza Mahakama kuwa Aprili 26 asubuhi alipokea simu na kuelezwa kuwa kuna tukio la mauaji Mwatulole, akatakiwa kwenda, alipofika alikuta mwili wa mwanamke ndani ya nyumba iliyokuwa haijamalizika kujengwa.

Ameieleza kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha mbalimbali, ikiwemo sehemu ya nyuma ya kichwa, mkono wa kulia huku kiganja kikiwa kimetenganishwa na mkono wa kulia na mkono wa kushoto kidole kimoja kikiwa kimekatwa na kitu chenye ncha kali.

Shahidi huyo ameeleza kuwa majeraha hayo yalikuwa makubwa, huku damu nyingi ilikuwa imetapakaa chini na kwamba wakati wa ukaguzi walibaini chupa ya fanta ikiwa na kimiminika kama maziwa pamoja na damu ukutani.

ASP Kijava alieleza kuwa baadaye alichukua sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba pamoja na alama za vidole kwenye chupa waliyoikuta eneo la tukio.

Mbali na Genja, ashtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 39/2023 ni Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55), ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe Seleman.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili Liberatus John (mshtakiwa wa kwanza), Laurent Bugoti anayemtetea mshtakiwa wa pili, Elizabeth Msechu anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Erick Lutehanga na Yesse Lubanda anayemtetea mshtakiwa wa tano.

Milembe Seleman (43), aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha ugavi katika kampuni ya GGML aliuawa Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani, usoni na mikononi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live