Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashahidi 34 kutoa ushahidi dhidi mauaji mwanafunzi Scolastica

10061 Pic+mwanafuzi TanzaniaWeb

Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jumla ya mashahidi 34 wa upande wa mashtaka watatoa ushahidi wao katika kesi ya mauaji ya kukusudia inayomkabili mmiliki wa Shule ya Scolastica, Edward Shayo na wenzake wawili.

Shayo pamoja mwalimu wa shule hiyo, Labani Nabiswa na mlinzi Hamis Chacha wanatuhumiwa kumuua mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo, Humphrey Makundi, Novemba 6, 2017.

Hata hivyo katika maelezo yote yaliyosomwa jana mahakamani hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji hayo isipokuwa maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa pili pekee, Chacha.

Maelezo hayo yalisomwa kuanzia nne asubuhi hadi saa tisa alasiri na wakili wa Serikali mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana aliyesaidiana na Lilian Kiweo na Nitike Emmanuel.

Katika maelezo yake ya ungamo anayodaiwa kuyatoa mbele ya mlinzi wa amani ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Irene Mushi, mshtakiwa huyo anadaiwa kukiri kumuua mtoto huyo.

Mlinzi huyo anaeleza katika maelezo hayo kuwa, Humphrey aliruka ukuta na wakati anamkimbiza alimpiga na ubapa wa panga mgongo na mara ya pili alimpiga usoni akaanguka.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Moshi, Julieth Mawolle, wakili huyo anaeleza kuwa baada ya kuanguka na kuhisi amefariki, mshtakiwa alimjulisha Nabiswa na baadaye alikuja Shayo na kusema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ukatupwe mtoni.

Maelezo ya mpelelezi mkuu wa kesi hiyo, Inspekta Waziri Tenga yanaeleza kuwa hakuna ubishi kuwa Shayo na Nabiswa walihusika kuficha taarifa hata baada ya kuokotwa kwa mwili.

Inspekta Tenga anaeleza katika maelezo hayo kuwa wakati mshtakiwa alipohojiwa na polisi, alikiri kumuua mwanafunzi huyo kwa kumpiga kwa ubapa la panga mgongoni na usoni.

Maelezo mengine yote ya mashahidi yanaeleza namna mwili huo ulivyogunduliwa mtoni, kuopolewa, kupelekwa hospitali ya mkoa ya Mawezi na baadaye kuzikwa na halmashauri.

Mbali na hilo, maelezo ya mashahidi wengine yanaeleza namna mwili wa mtoto huyo ulivyofukuliwa na kufanyiwa uchunguzi (postmoterm) katika Hospitali ya KCMC.

Pia upo ushahidi wa mtaalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Hadija Mwema ambaye alichunguza sampuli zilichokuliwa kwenye mwili uliofukuliwa na kuzioanisha na za wazazi wake.

Kwa upande wake, baba mzazi, Jackson Makundi katika maelezo yake anaeleza namna alivyopata taarifa za mwanaye kutokuwwpo shuleni kuanzia Novemba 7, 2017 na jitihada za kumtafuta. Kesi hiyo iliahirishwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz