Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashahidi 24, vielelezo 58 dhidi ya kina Kisena

Kisena Pic Data Mashahidi 24, vielelezo 58 dhidi ya kina Kisena

Wed, 27 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Tanzania inatarajia kuwaita mashahidi 24 na kuwasilisha vielelezo 58 katika kesi moja kati ya tatu za uhujumu uchumi zinazomkabili mkurugenzi wa mradi wa Usafirishaji wa Mabasi yaendayo haraka, maarufu kama mwendokasi (UDART), Robert Kisena na wenzake.

 Serikali imebainisha idadi umetaja idadi hiyo ya mashahidi na vielelezo hivyo, leo Jumatano, Julai 27, 2022 wakati ikiwasomea washtakiwa hao maelezo ya mashahidi wanaotarajiwa kuitwa.

Katika kesi hiyo namba 20, iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Pamela Mazengo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, katika hatua ya uchunguzi wa awali, Kisena na wenzake kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 15.

Mbali na Kisena mwenye umri wa miaka 47, ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Simon Group Ltd, washtakiwa wengine ni Charles Newe ( 48) mkurugenzi wa Udart, mfanyabiashara John Samangu ( 66) na mtunza fedha wa Udart,  Tumaini Kulwa( 44).

Mashtaka hayo yanayowakabili ni pamoja na kuongoza genge la uhalifu, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, utakatishaji fedha haramu na kuisababishia Udart hasara ya Sh750, milioni, wakidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei 25 na Julai 10, 2016.

Wanadaiwa walihamisha pesa hizo kutoka katika akaunti ya Udart katika benki ya NMB, tawi la Bank House, kwenda akaunti ya kampuni ya Long Way Engineering Ltd iliyoko Benki ya KCB.

Wanadaiwa kuhamisha pesa hizo kwa madai ya kutumia kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mabasi na uzio katika maeneo la Kimara, Kivukoni, Ubungo na Moroco, wakati wakijua sio kweli.

Hatua hiyo ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi, imehitimisha jukumu la mahakama hiyo ya Kisutu na kufunga jalada hilo ambapo sasa imetoa amri ya kuhamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambako ndiko itakakosikilizwa na kuamuriwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live