Mashahidi 15 wa upande wa mashtaka wanatarajia kutoa ushahidi wao, katika kesi ya kuchapisha maudhui yanayokiuka haki na uhuru wa mtu mwingine, inayomkabili Mkurugenzi wa mtandao wa U-turn Collection, Allen Mhina (31) na wenzake wawili.
Hiyo ni baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na washtakiwa kusomewa hoja za awali (PH) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbali na Mhina, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 57/2022 katika Mahakama hiyo ni Mtandao wa U-turn Collection na Mange Kimambi App.
Kwa pamoja wanaokabiliwa na mashtaka matatu yakiwemo ya kuchapisha maudhui yanayokiuka haki na uhuru wa mtu mwingine na kumfedhesha mtu kwa njia ya mtandao (cyber bullying).
Washtakiwa hao wamesomewa hoja zao Jumatano Aprili 27, 2022 na wakili wa Serikali Adolf Lema akishirikiana na Mwanaamina Eddie, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.
Advertisement Mhina baada ya kusomewa hoja zake, alikiri kuwa yeye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa U-turn Collection na kwamba umesajiliwa Brela na amepewa leseni ya kuendeshea maudhui mtandaoni na TCRA Septemba 22, 2021.
Alikiri kuwa mtandao wa U-turn unajihusisha na kazi mbalimbali za ubunifu na burudani na yeye ndio anayesimamia shughuli zote zinazofanywa na Mange Kimambi App.
Mhina anayetetewa na wakili Abubakari Salimu alikiri kuwa alifikishwa mahakamani hapo Aprili Mosi, 2022 kujibu mashtaka yanayomkabili, huku akikana hoja nne.
Hata hivyo upande wa mashtaka walidai kuwa wanatarajia kupeleka mahakamni hapo mashahidi 15 na hivyo kuiomba mahakama hiyo ipange terehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate anayesikikiza shauri hilo, baada ya kusikiliza maeleoz hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni Mosi, 2022 itakapoanza kusikilizwa ushahidi.
"Kesi hii itasikikizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Juni Mosi hadi Juni 3, upande wa mashtaka mjitajiid kuleta mashahidi" amesema Hakimu Kabate .
Katika kesi ya msingi, Washtakiwa wanadaiwa kuchapisha maudhui yanayokiuka haki na uhuru wa mtu mwingine Machi 9, 2022 katika maeneo tofauti ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Siku hiyo ya tukio, wanadaiwa walichapisha video ya aliyekuwa Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) maudhui ambayo yanadhuru haki ya faragha ya mgonjwa.
Shtaka la pili, ni kufanya kazi ya uandishi wa habari bila ya kuwa na kibali kutoka bodi ya ithibati ya wanahabari, shtaka linalomkabili Mhina na mshtakiwa wa pili (U-turn Collection).
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Septemba 22, 2021 na Machi 14, 2022 Kinondoni eneo la Manyanya, ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila ya kuwa na kibali kutoka bodi ya ithibati ya wanahabari.
Shtaka la tatu ni kumfedhesha mtu kwa njia ya mtandao (cyber bullying), shtaka linalomkabili Mhina peke yake.
Anadaiwa kutenda kosa hilo, Machi 9, 2022 katika maeneo tofauti ndani ya nje ya nchi ya Tanzania.
Mhina kupitia mfumo wa kompyuta unaojulikana kama Mange Kimambi APP, unaosimamiwa na U-turn Collection alichapisha video ya aliyekuwa Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu Profesa Jay ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha wagonjwa Mahututi (ICU) kwa nia ya kusababisha dhiki ya kihisia (emotional distress)