Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka watoto watatu wa familia moja waliochinjwa Njombe

39465 Pic+njombe Mapya yaibuka watoto watatu wa familia moja waliochinjwa Njombe

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Njombe. Danford Nziku, baba wa watoto watatu waliotekwa na kukutwa wakiwa wamechinjwa wilayani Njombe amedai chanzo cha watoto wake kuuawa ni ugomvi kati yake na mtoto wa marehemu kaka yake.

Watoto hao; Godliva Mwenda (11), Gasper Nziku (8) na Giliad Nziku (5) walichukuliwa na mtu anayedaiwa kuwa ni Joely walipokuwa wakicheza nyumbani kwao katika Kijiji cha Ikando, Kata ya Kichiwa ambako walichinjwa kisha kunyofolewa viungo bvya mwilini.

Danford alisema kwa takribani mwaka mmoja na nusu, amekuwa kwenye ugomvi na Joely ambaye sasa anashikiliwa na Polisi. Alisema ndugu yake huyo amekuwa akimtuhumu kuwa amemroga.

“Huyu jamaa (Joely) alianza chokochoko akisema anaumwa lakini mimi sitaki kumuuguza, hivyo siku moja akaja hapa nyumbani akasema mimi na ndugu zangu tuondoke kwenye mji huu,” alisema Nziku.

“Nilishangazwa kumsikia akisema hayo. Wakati huyu jamaa nimemlea tangu akiwa mdogo baada ya baba yake (kaka yangu) kufariki, kama ningekuwa mchawi si ningemroga wakati huo, iweje leo mtu ana maisha yake na kwangu ameondoka.”

Alisema kuna siku Joely alikwenda nyumbani kwake akiwa na tairi la gari akiwa na lengo la kuchoma moto lakini bahati nzuri hakumkuta na alipopata taarifa hizo alitoa taarifa ofisi ya Serikali ya kijiji.

“Mimi nikaenda Ofisi ya Serikali kutoa taarifa ndipo alipoitwa na alipobanwa sababu za kupeleka tairi nyumbani kwangu wakati hatupatani, alikiri kwamba alitaka kunichoma moto kwa madai ya uchawi.”

Alisema Joely aliendelea na visa na Januari 20, akiwa na mkewe walirejea nyumbani usiku na kukuta watoto wote hawapo na milango ya nyumba zote mbili ikiwa wazi.

Alisema waliwatafuta maeneo ya jirani bila mafanikio na baadaye wakaenda kwa jirani yao kuulizia, wakamkuta mtoto mmoja ambaye jioni hiyo walikuwa wote nyumbani wakicheza na aliwaeleza kwamba wakati wakiwa nyumbani hapo alikuja mtu waliyemtambua kwa jina la Joely na kuondoka na watoto hao.

Alisema baada ya maelezo hayo wakaondoka kwenda nyumbani kwa wazazi wa mtoto wa pili ambaye walikuwa naye wakati huo ambaye pia aliwaeleza kuwa watoto wake wamechukuliwa na Joely kwenda Makambako.

Nziku alisema alishikwa na butwaa kusikia Joely ndiye aliyewachukua watoto wake wakati haelewani na hata siku moja hajawahi kufika nyumbani kwake tangu watofautiane.

Alisema alikwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na usiku huohuo walifunga safari kwenda Makambako kutoa taarifa polisi ambao walikwenda kumkamata Joely kabla ya kufanya upekuzi ndani ya nyumbani yake bila mafanikio.

Alisema baada ya kutoa taarifa polisi waliendelea na msako wa kuwatafuta watoto hadi Jumapili ya Januari 27, walipoambiwa na polisi kwamba kuna watoto wameokotwa huku wakiwa wamefariki hivyo waende mochwari ya Hospitali ya Kibena kuwatambua na walipofika waliwatambua kuwa ni watoto wao.

Maisha bila watoto

Nziku anasema kwa sasa maisha yake yatakuwa magumu mno baada ya kuondokewa na watoto wake ambao walikuwa tegemeo kwake akisema walikuwa wakimsaidia shughuli ndogondogo za nyumbani.

“Nilizoea kusaidiana nao siku zote iwe kuchunga mbuzi, kufungulia na kufungia kuku kama mimi na mama yao tunapochelewa kurudi nyumbani, lakini sasa hata ndoto za shule zimekoma kwa kuchinjwa kikatili.”

Mkazi wa Kijiji hicho, Marcus Mwinami alisema wanafahamu ugomvi wa wawili hao akiishukuru Serikali kwa kazi nzuri katika kushughulikia tukio hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz