Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka wanaoumiza wafanyabiashara wa tanzanite

418af7cc597509349a079f6167c9befa Mapya yaibuka wanaoumiza wafanyabiashara wa tanzanite

Sun, 3 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHI la Polisi mkoani Arusha limekiri kuwa mtandao wa kutapeli wafanyabiashara ya madini ya tanzanite katika mikoa ya Arusha na Manyara ni wa hatari.

Hayo yalibainishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Salumu Hamduni, alipozungumza na Habari Leo jana.

Kamanda Hamduni alisema kwa kuwa mtandao huo, una watu wengi na wengine wanatoka nje ya Mkoa wa Arusha. Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi kwa umakini zaidi, ili kuwakamata wote wanaohusika na mtandao huo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Hivi karibuni Kamanda Hamduni alisema watu sita akiwemo mfanyabiashara maarufu wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Lucas Mndeme (46) na askari polisi watatu, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kushawishi na kuomba rushwa ya zaidi ya Sh milioni 30.

Alisema watu hao wanadaiwa kuomba rushwa hiyo kutoka kwa Sammy Mollel, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya kununua na kuuza madini ya Gem and Rock Venture kwa madai anakwepa kulipa kodi na anafanya biashara ya madini ya tanzanite kwa njia ya magendo.

Hamduni alisema tukio hilo ni la Desemba 14, mwaka huu katika ofisi ya Gem and Rock Venture iliyopo Mtaa wa Pangani Kata ya Kati jijini Arusha.

Aliwataja askari polisi hao ni G.5134 Konstebo Heavenlinght Mushi wa Kitengo cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, H 1021 Konstebo Bryton Murumbe askari polisi kazi za kawaida wa Mkoa wa Dodoma na H.125 Konstebo Gasper Paul, askari polisi wa Kitengo cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma.

Kamanda Hamduni alisema kikosi hicho ni hatari na ndiyo maana polisi iko makini katika uchunguzi, ili wote waliohusika wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria, kujibu mashtaka yanayowakabili.

Alisema Jeshi la Polisi bado linawashikiliwa polisi wanaotuhumiwa kuhusika na tuhuma hizo na hawajapewa dhamana, bado wako rumande, kwa sababu wanatakiwa kwanza kushitakiwa kwenye mahakama ya kijeshi kisha kupelekwa kwenye mahakama ya kiraia.

"Hata sisi polisi tumeambiwa hiki kikosi ni hatari sana; na kina watu wengi sana, hivyo hata sisi tunafanya uchunguzi kwa makini sana na wote waliohusika watakamatwa ili kuvunja mtandao huu," alisema Kamanda Hamduni.

Kamanda Hamduni alikiri kumwachia kwa dhamana mfanyabishara Mndeme. Alisema kuwa dhamana ni haki yake kisheria.

Kamanda Hamduni alisema wengine waliokamatwa ni mfanyabiashara na mkazi wa Makole Dodoma, Shabani Benson (40), Leonia Joseph (40) mkazi wa Ilboru ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Gem and Rock Venture na Joseph Chacha (43) mkazi wa llboru.

Wengine ni Omary Mario (43) mfanyabiashara na mkazi wa Olorien Arusha, Nelson Lyimo (58) mfanyabiashara na mkazi wa Kimandolu jijini Arusha.

Chanzo: habarileo.co.tz