Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka mume kudaiwa kumuua mke kwa kisu

Amina Mauaji Mapya yaibuka mume kudaiwa kumuua mke kwa kisu

Wed, 7 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati Jeshi la Polisi likimsaka Mshaka Jeremia kwa tuhuma za kumuua mkewe Amina Hasasan kwa kumchoma kisu sehemu tofauti za mwili, mwenyekiti wa mtaa wa Mkoani walikokuwa wakiishi wana ndoa hao, Salvatory Paulo amesema mgogoro wa ardhi kati ya wawili hao inaweza kuwa miongoni mwa sababu za mauaji hayo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuuaga mwili wa Amina uliosafirishwa kwenda mkoani Dodoma kwa mazishi, mwenyekiti huyo alisema Agost 18, mwaka huu, mwanaume huyo aliwasiliha ofisini kwake lalamiko la mkewe kuuza moja ya viwanja vya familia bila rdihaa yake, suala lililosuluhishwa na kumalizika.

“Baada ya mke kukiri kuuza kiwanja hicho kwa Sh7 milioni kwa ajili ya kulipia gharama za shule kwa mtoto wao kutokana na mume kuondoka nyumbani bila kurejea kwa kipindi kirefu, suala hilo lilisuluhishwa na wote wawili kuafikia kulimaliza; kumbe inaonekana mwanaume ulikubali shingo upande,” alisema Paulo

Akifafanua suala hilo, mwenyekiti huyo alisema baada ya kuuza, Amina ambaye sasa ni marehemu alitumia Sh2 milioni kulipia gharama za elimu ya mtoto wao, huku Sh5 milioni zilizosalia alizihifadhi na kumkabidhi mume wake aliporejea nyumbani.

“Hii inadhihirisha wazi kuwa mama huyu hakuuza kiwanja kwa nia mbaya zaidi ya kugharamia elimu ya mtoto wao,” alisema Paulo

Alitumia fursa hiyo kuwaasa kinamama kuwashirikisha waume zao kwenye maamuzi makubwa yanayohusu mali za familia, huku akiwasihi kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali na ikibidi kuondoka kwenye ndoa iwapo kuna ishara za kuhatarisha maisha na uhai wao.

Mmoja wa marafiki wa marehemu Amina, aliyezungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina alisema mgogoro kati ya rafiki yake na mumewe ulianza baada ya mmoja wa watoto wao kuhitimu darasa la saba na mama kuamua kumpeleka shule binafsi kuendelea na elimu ya sekondari.

"Wakati huo mwanaume alikuwa huko migodini ndipo mke alipoamua kuuza moja ya viwanja vyao kwa Sh7 milioni na kutumia Sh2 milioni kumlipia mtoto shule na kuhifadhi Sh5 milioni zilizobaki hadi mume wake aliporudi," alisema.

Chanzo: Mwananchi