Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka mama aliyeua watoto wake kwa sumu

Siripic Data Mapya yaibuka mama aliyeua watoto wake kwa sumu

Sat, 4 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Veronica Gabriel (30), mkazi wa Kijiji cha Mwabagaru wilayani Chato kwa tuhuma za kuwanywesha sumu watoto wake watano kabla ya yeye mwenyewe kunywa sumu hiyo akilalamikia ugumu wa maisha.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe ilisema mama huyo aliwanywesha watoto wake sumu ya kunyunyizia nyanya kuua wadudu aina ya incecron profenos 720g/L na kusababisha kifo cha watoto wake wawili.

Hata hivyo, Diwani wa Buseresere, Godfrey Miti ameliambia Mwananchi kuwa alipata taarifa za tukio hilo baada ya kupigiwa simu na mwenyekiti wa kijiji aliyekuwa eneo la tukio.

“Mwenyekiti naye alipata taarifa kutoka kwa watu waliokuwa wamepita jirani na nyumba hiyo na kusikia harufu kali ya dawa ya kuua wadudu kwenye pamba na ndani ya nyumba kukawa kama kuna kelele, wakaamua kuingia ndani na kukuta tayari mama huyo ameshawapa sumu watoto wake pamoja na kunywa yeye mwenyewe. Ndipo wakampigia simu mwenyekiti,” alisimulia diwani huyo.

Baada ya kupata taarifa hizo, alisema alitafuta usafiri ili wawahishwe hospitali. “Lakini wakati tunahangaikia usafiri, tayari watoto wawili walikuwa wameshafariki na wengine hali zao zilikuwa mbaya,” alisema Miti.

Kwa mujibu wa diwani huyo, Veronika alitekeleza tukio hilo kwa madai ya kuishi maisha magumu.

Advertisement “Nilimhoji mwenyekiti wa kijiji kama kweli mama huyu alikuwa na maisha magumu kiasi cha kuamua kufanya tukio hilo akasema hapana.

“Hata mimi ninavyofahamu, huyu mama hakuwa na maisha magumu kiasi cha kumfanya achukue uamuzi wa kuua familia yake,” alisema.

Maisha ya Veronika

Akizungumzia maisha ya Veronika, Diwani Miti alisema alikuwa na mashamba ambayo alikuwa akiyahudumia na kupata mazao ya kumudu maisha na familia yake.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa hakuwa na mume na aliihudumia familia peke yake, tayari kata ilikuwa imeshamuingiza kwenye Mpango wa Kuhudumia Kaya Masikini (Tasaf) mwaka huu ili anufaike na fedha zinazotolewa kama walivyo wenzake wasio na msaada wa ndugu.

“Binafsi nimesikitika kwa kitendo alichokifanya huyu mama. Kama alikuwa na shida kubwa, angefika ofisi ya kijiji au kata kuomba msaada. Tusingeshindwa kumsaidia japo chakula. Hatujafikia hatua mbaya ya kushindwa kuwasaidia wananchi wetu hata chakula,” alisema Miti.

Diwani huyo alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuacha kujichukulia hatua mkononi pale wanapokabiliwa na matatizo ya kimaisha, bali wawashirikishe viongozi wa Serikali kupata msaada muhimu utakaowasaidia kuzikabili changamoto walizonazo.

Inaelezwa kuwa Veronika amewanywesha sumu watoto wake watano wenye umri wa kati ya miaka 12 na miezi tisa.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwaibambe, watoto waliofariki dunia ni aliyekuwa na miaka 12 na mwingine wa miaka miwili.

“Watoto wengine wamelazwa Kituo cha Afya Bwanga na mama yao ambaye kwa sasa ni mtuhumiwa na yuko chini ya ulinzi wa polisi,” alisema kamanda huyo.

Afya yake itakapoimarika, Veronica atachukuliwa hatua za kisheria kwa kitendo hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live