Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka kesi ya askari wanaodaiwa kumuua muuza madini

Watuhumiwa Mtwara (600 X 590) Mapya yaibuka kesi ya askari wanaodaiwa kumuua muuza madini

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara imeelekeza mabaki ya mifupa ya marehemu Mussa Hamis iliyowasilishwa na kupokewa mahakamani hapo kuwa vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayowakabili askari Polisi saba mkoani Mtwara, yatunzwe kwa utu na mahali salama.

Maelekezo hayo yametolewa na Jaji Edwin Kakolaki, anayesikiliza kesi hiyo akitokea Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo Jumatano, Novemba 29, 2023, baada ya shahidi wa nane na pekee wa upande wa mashtaka kwa leo kuhitimisha ushahidi wake.

"Kwa kuwa ni viungo vya binadamu vinahitaji kutunzwa kwa utu na mahali salama", amesema Jaji Kakolaki na kuongeza kuwa hivyo kwa leo vielelezo hivyo vitabaki katika mikono ya Mahakama hadi hapo kesho itakapotoa maelekezo mengine kuhusu mahali pa kuvihifadhi.

Mahakama imetoa maelekezo hayo kufuatia hoja iliyowasilishwa na kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Maternus Marandu, baada ya shahidi wa nane, aliyeiwasilisha mahakamani hapo mifupa hiyo, kuhitimisha ushahidi wake.

Shahidi huyo Fidelis Charles Bugoye, Mkemia wa Serikali Mwandamizi, kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ndiye aliyefanya uchunguzi wa vinasaba vya mifupa hiyo na kulinganisha na vinasaba kwenye sampuli ya mate ya mama wa marehemu Mussa, Hawa Bakari Ally.

Wakili Marandu aliiomba Mahakama kuwa kwa vielelezo hivyo ni mabaki ya viungo vya binadamu vinapaswa kuhifadhiwa mahali maalumu wakati kesi hiyo itakapokuwa inaendelea mpaka hapo mahamam itakapotoa maelekezo mengine.

Wakili Marandu amependekeza kuwa mahali sahihi ni ofisi ya Mkemia Mkuu wa Sekali lakini akaomba kwa leo vipelekwe katika kituo cha Polisi kabla ya kesho askari Polisi kufanya utaratibu wa kuvihamisha kwenda kuvikabidhi ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Naye kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu ameunga mkono kuwa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni mahali sahihi pa kuhifadhi vielelezo hivyo.

Hata hivyo, Wakili Magafu ametahadharisha kuwa kulingana na unyeti wa vinatakiwa kukabidhiwa katika ofisi hiyo moja kwa moja badala ya kuvipeleka Polisi kwanza, huku akitoa hoja kwamba shahidi aliyeviwasilishwa ndiye anapaswa kukabidhiwa avipeleke tena kwa maandishi.

Wakati Wakili Magafu akitoa hoja hiyo shahidi huyo, alikuwa ameshatoka nje ya ukumbi wa Mahakama baada ya kuhitimisha ushahidi wake.

Lakini hata askari Polisi pamoja na mmoja wa waendesha mashtaka walipokwenda kumuangalia nje hakupatikana, tayari alishaondoka eneo la Mahakama na hakupatikana kwenye simu.

Kutoka na hali hiyo ndipo Jaji Kakolaki akaelekeza vielelezo hivyo vibaki katika mikono ya Mahakama kwa leo hadi kesho utakapofanyika utaratibu mwingine.

Awali katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Chivanenda Luwongo, Fidelis Charles Bugoye ameieleza mahakama hiyo kuwa ndiye aliyefanya uchunguzi wa mifupa ya mbavu na ya miguu iliyopatikana mahali ambako mwili wa Mussa ulitupwa baada ya kuuawa.

Shahidi huyo ameeleza kuwa pia alifanya uchunguzi wa vinasaba kutoka katika mpanguso mama wa marehemu Mussa, Hawa Bakari Ally na kwamba matokeo ya mpangilio wa vinasaba katika mifupa hiyo ulifanana na mpangilio wa vinasaba katika mpanguso (mate) ya mama wa marehemu.

Kwa mujibu wa shahidi wa tatu, Kamishna wa Polisi Msaidizi (ACP) Yustino Mgonja, waliamua kupeleka mifupa hiyo pamoja na sampuli ya mate ya mama wa marehemu Mussa kwa Mkemia kwa uchunguzi wa vinasaba ili kujiridhisha kama Mussa ambaye alikuwa akitafutwa na ndugu zake ndiye huyo aliyekuwa ameshafariki.

Wakati wa tukio hilo, ACP Mgonja ambaye kwa sasa ni Kamanda wa Polisi mkoa (RPC ) wa Ilala Dar es Salaam, alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa Mtwara na ndiye aliyekuwa Kiongozi wa timu ya wapelelezi wa kesi hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi (Insp.) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Wanadaiwa kumuua kwa maksudi Mussa Hamis Januari 5, 2022 katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, na kwenda kuutupa mwili wake katika kijiji cha Majengo Kata ya Hiari karibu na kiwanda cha Sementi cha Dangote.

Wanadaiwa kumuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi, ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizozichukua walipokwenda kumpekua nyumbani kwao, kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea, Lindi; wakimtuhumu wizi wa pesa na pikipiki.

Alichokieleza shahidi katika ushahidi wake.

Awali katika ushahidi wake Bugoye ameeleza kuwa majukumu yake ni kupokea vielelezo mbalimbali vya jinai vikiwemo vinavyohitaki uchunguzi wa vinasaba (DNA), uchunguzi wa sumu, uchunguzi wa madawa ya kulevya, kuvifanyia uchunguzi, kuandaa taarifa ya uchunguzi na kutoa ushahidi mahakamani pale inapohotajika.

Kuhusiana na kesi hiyo amesema kuwa Januari 27, 2022 akiwa ofisa wa zamu katika kituo chake cha kazi Dar es Salaam, alipokea ofisa mkemia kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kusini, Mtwara ambaye aliwasilisha vifurushi mbalimbali.

Kwa mujibu wa maelezo ya ushahidi wake vifurushi hivyo vilivyokuwa vimefungwa kwa lakiri ndani vilikuwa na vielelezo mbalimbali, huku vikiwa vimepewa majina ya herufi kuanzia A, ambayo ilikuwa mifupa minane ya mbavu iliyodhaniwa kuwa ya binadamu

Kifurushi B kilikuwa ni mifupa miwili ya mguu iliyodhaniwa kuwa ya binadamu, D ilikuwa suruali iliyokutwa eneo la tukio, yenye rangi ya kijani ikiwa na udongoudongo.

Kifurushi F kilikuwa na mpanguso wa kinywa (mate kutoka ukuta wa ndani wa shavu) kutokuwa kwa Hawa Bakari Ally, mama wa marehemu Mussa na C ulikuwa na funza, waliochukuliwa eneo la tukio ulikotupwa mwili wa marehemu Mussa.

Mbali na vifurushi hivyo vyenye vielelezo, kulikuwa na barua kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kusini, Mtwara ya Januari 25, 2022 pamoja na barua kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) Mtwara na PF180 ya Januari 24, 2022.

Barua ile ya Polisi ilikuwa inamtaka shahidi huyo kufanya uchunguzi wa vile vielelezo A (mifupa ya mbavu), B ( mifupa ya mguu) na D (suruali) kama vina mahusiano ya vinasaba na kielelezo F (mpanguso wa mate wa Hawa Bakari Ally, mama wa marehemu Mussa).

Kwa upande wa kielelezo C (funza) barua hiyo ilikuwa inamtaka kuchunguza kama kulikuwa na sumu.

Mkemia Mkuu wa Serikali siku hiyohiyo alitoa maelekezo kwa mkurugenzi na Mkurugenzi akayawasilisha maelekezo hayo kwake kuwa uchunguzi ufanyike.

Hivyo alichukua vielelezo vilivyohitaji uchunguzi wa vinasaba yaani A, B, D na F, akaenda kwenye maabara ya vinasaba kuanza uchunguzi, wa awali kujiridhisha kwanza kama hiyo mifupa ni ya binadamu.

Katika hatua hiyo alichukua sampuli kutoka katika vielelezo A na B yaani vipande vidogo vya mifupa ile ya mbavu na ya miguu hivyo jumla ya sampuli 10 (vipande 8 kila mfupa wa mbavu) na viwili katika mifupa ya mguu.

Katika uchunguzi huo aliotumia vifaa kemikali na njia za Kisayansi, matokeo ya sampuli za kielelezo A (mbavu) alijiridhisha kuwa ni mifupa ya binadamu.

Hata hivyo, katika kielelezo B (mifupa ya mguu) pamoja na kielelezo D (suruali) hakuendelea na uchunguzi wake kwa sababu hakuweza kupata kiwango cha kutosha cha vinasaba.

Hivyo baada ya uchunguzi wa awali wa kubaini kama ile ilikuwa ni mifupa ya binadamu sasa aliingia katika uchunguzi wa vinasaba

Matokeo ya uchunguzi huo wa vinasaba yalionesha kuwa sampuli za kielelezo A ni vya umiliki wa mtu wa jinsia ya kiume na kwamba sampuli za kielelezo F ni mtu wa jinsia ya kiike.

Kuhusu matokeo ya mpangilio wa vinasaba matokeo hayo yalionesha kuwa A (mifupa ya mbavu) katika Maeneo yote 15 ya mpangilio wa vinasaba yalifanana na maeneo yote 15 ya mpangilio wa vinasaba katika kielelezo F (mate ya Hawa Bakari Ally)

"Hivyo uwezekano wa Hawa Bakari Ally kuwa mama mzazi wa Mussa Hamis ni asilimia 99.9," amesema, Bugoye.

Baada ya maelezo hayo shahidi huyo ndipo akaiomba Mahakama nayo ikaipokea mifupa hiyo ya mbavu ya mguu, suruali na ripoti ya matokeo ya uchunguzi kuwa vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka.

Maswali ya dodoso

Baada ya ushahidi wake wa msingi shahidi huyo amehojiwa maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi kama ifuatavyo:

Wakili Magafu: Shahidi, hiyo barua ya kutoka Mtwara kuomba uchunguzi umeitoa hapa mahakamani?

Shahidi: Sijaitoa.

Wakili: Uliwahi kuandika maelezo yako kuhusiana na hii kesi?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Hiyo reference number yake (namba ya kumbukumbu ya barua) unaikumbuka?

Shahidi: Siikumbuki maana ni.muda mrefu.

Wakili: Mbona asubuhi ulikuwa unaikumbuka kwa nini sasa hivi huikumbuki?

Shahidi: Sasa hivi siikumbuki kwa sababu kichwa changu kina mambo mengi.

Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba asubuhi ulikumbuka kwa sababu uliiandika kwenye kiganja chako na ulikuwa inasoma kwenye kiganja?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Kwa nini hukuona umuhimu wa kuja na hiyo barua ili mahakama ione kile ulichoelekezwa kufanya?

Shahidi: Sikuja nayo kwa sababu sikuandikiwa mimi aliandikiwa Mkemia Mkuu wa Serikali na mimi sijatakiwa kuja nayo hapa.

Wakili: Umesema ulifanya uchunguzi hebu twambie ni utaratibu gani unatumika kuchukua sampuli kwa mtu aliye hai na kwa sheria gani?

Shahidi: Si mimi niliyechukua sampuli.

Wakili: Lakini wewe kama mtaalmu tuambie utaratibu ukoje na ni sheria gani inatumika?

Shahidi: Ni sheria ya Vinasaba vya Binadamu namba 4 ya mwaka 2009.

Wakili: Sasa hebu tusaidie mnatumia utaratibu gani ukitaka kuchukua mate au damu ya mtu?

Shahidi: Utaratibu umeelezwa kwenye hiyo sheria.

Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba kwenye hiyo sheria kuna fomu ambayo utatakiwa ujaze?

Shahidi: Mimi si mtaalamu wa sheria.

Wakili: Kwenye hiyo barua ilimtaja nani alichukua hiyo sampuli kutoka kwa Bi Hawa (mama wa marehemu)?

Shahidi: Haikumtaja.

Wakili: Hebu angalia hiki kielelezo, maelezo yake kama kuna jina la mtu aliyechukua sampuli hizo za Hawa?

Shahidi: Sijamtaja

Wakili: Shahidi, asubuhi tumekusikiliza sana ukielezea utaraibu wote ulioutumia wakati unafanya uchunguzi, kwenye hayo maelezo yako uliwahi kuandika ulivyofanya mpaka ukafikia hitimisho?

Shahidi: Sikuandika

Wakili: Hiki ni kielelezo PE 9 ni kitu gani?

Shahidi: Ni taarifa ya uchunguzi uliofanyika.

Wakili: Ulifanywa na nani?

Shahidi: Na mimi.

Wakili: Shahidi wakati unatoa ushahidi wako ulisema kuna njia tofauti za kupata matokeo ya DNA, siyo?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ziko ngapi kama unaweza kukumnbuka, tano, saba au nyingi tu?

Shahidi: Ziko nyingi tu.

Wakili: Wewe ulitumia njia gani?

Shahidi: Kwenye hatua gani?

Wakili: Hatua ya profiling (mpangilio wa vinasaba)

Shahidi: Hiyo ni hatua ya mwisho ambayo inatumika kwenye mtambo.

Wakili: Je, kwenye hiyo ripoti yako hicho unachokisema kinaakisi kwenye ripoti hiyo?

Shahidi: Hakikuhitajika kuwepo maana hii si njia ya uchunguzi bali ni taarifa ya uchunguzi.

Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba katika ripoti ya Kisayansi lazima iambatane na findings zake?

Shahidi: Findings kwa maana ya matokeo ya uchunguzi nakubaliana na wewe.

Wakili: Utakubaliana na mimi kwenye hiyo ripoti yako unachoonesha ni conclusion (hitimisho) tu ya kile ulichokipata?

Shahidi: Kwenye ripoti yangu kuna matokeo ya uchunguzi.

Wakili: Lakini hakuna findings (matokeo)?

Shahidi: Findings ni njia.

Wakili: Ndio tusifanye kama tunakariri tu. Ni namna gani ulifikia hayo matokeo hayapo?

Shahidi: Hiyo mifupa uliwahi kujua ni ya mwanaume wa umri gani?

Shahidi: Uchunguzi haukuhitaji kujua umri wa mtu.

Wakili: Na wala uchunguzi haukuhitaji kujua kama alikuwa wa kime au mwanaume?

Shahidi: Uchunguzi ulihitaji vinasaba katika vinasaba unajua jinsia.

Wakili: Hiyo humu umeiandika kwamba alikuwa mwanaume au mwanamke?

Shahidi: Ndio (anasoma kwenye ripoti yake hiyo sehamu aliyobaimosha jinsia kuwa ilikuwa mifupa ya mwanaume).

Wakili: Wakati unatuonesha hapa zile mbavu ulionesha ni sehemu gani ya hiyo mifupa ulikwangua (kupata sampuli) ya kwenda kufanyia uchunguzi?

Shahidi: Sikuulizwa hilo swali.

Wakili: Na Vilevile kwenye hiyo miguu hukuonesha?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Na kwenye suruali ulifanyaje ulikataa kipande au uliweka yote?

Shahidi: Nilikata kipande kidogo naweza kuonesha.

Wakili:Na ulijua hizi mbavu zinasadikiwa za Mussa Hamis sababu iliandikwa kwenye barua kweli au si kweli?

Shahidi: kweli.

Wakili: Ni kweli kwa sababu ulishatanguliziwa majibu

Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba Ukiachilia mbali kupewa jina la Mussa Hamis kusema mwanaume anawza kuwa kaka au baba yake, mzazi au mtu yeyote ambaye ni wa kiume?

Shahidi: Kwa uchunguzi huu maeneo yote 15 kielelezo A (mifupa ya mbavu) yalilingama na 15 ya kielelezo F (mate ya mama wa Musa) maana yake kuna uhusiano.

Wakili: Hicho umekisema kwenye ripoti yako hii?

Shahidi: Hayo si sehemu ya ripoti

Wakili: Kama wewe usingewekuwepo labda ingekuwa umekwenda masomoni mtu mwingine hapa angeweza kuvundua hicho unachokisema?

Shahidi: Mtu mwingine asingeweza lakini mtaalamu angeweza.

Wakili: Sasa hiyo mifupa miwili ni ya mguu upi?

Shahidi: Ukiitazama ile ni mguu wa kulia.

Wakili: Ni kitu gani kinaweza kutofautisha kuwa huu ni mfupa wa binadamu na si wa nyani?

Shahidi: Nilieleza kwenye ushahidi wangu kwamba nilifanya uchungzi wa awali nikagundua kuwa ni mifupa ya binadamu.

Wakili: Kuna tofauti gani kati ya ripoti na conclusion (hitimisho)?

Shahidi: Hitimisho ni sehemu ya ripoti.

Wakili: Utakubaliana nami kwamba hiyo siyo ripoti bali ni conclusion?

Shahidi: Hapana ni ripoti na ina conclusion.

Wakili: Haya Mheshimiwa atasom maana naye ameshafanya ma-research (utafiti) mengi tu.

Wakili Robert Dadaya: Shahidi, katika vielelezo ulivyopokea kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kulikuwa na kielelezo C, si ndio?

Shahidi: Ndio

Wakili: Ambao ni funza si ndio?

Shahidi: Ndio

Wakili: Ulipata kujua funza hao walitoka wapi?

Shahidi: Eneo la tukio (ulikotupwa mwili wa marehemu Mussa).

Wakili: Sijasikia kuhusiana na taratibu za uchunguzi wa wale funza unaweza kuieleza mahakama japo kidogo na matokeo yake?

Shahidi: Baada ya uchunguzi matokeo yalionesha kuwa hapakuwa na sumu (baada ya kuelezea utaratibu wa uchunguzi wa sampuli hiyo ya funza).

Wakili: Baada ya uchunguzi huo uliandaa ripoti?

Shahidi: Ndio niliandaa ripoti ya uchunguzi huo.

Wakili: Umeiwasilisha hapa mahakamani kama kielelezo?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Ungependa kuitoa kama kielelezo maana bila shaka unaiamini?

Shahidi: Ni ripoti yangu hivyo inaweza kutumika kama kielelezo.

Jaji Kakolaki: Ripoti hii imepokewa na kuwa kielelezo cha tatu cha upande wa utetezi (DE3)

Maswali ya ufafanuzi kutoka kwa Wakili Marandu:

Wakili: Shahidi umeulizwa kama uliandika procedure (taratibu) za uchunguzi kwenye ripoti yako lakini ukajibu kuwa hukuandika hebu fafanua.

Shahidi: Taratibu za uchunguzi unataja kile unachotaka, aliyeomba uchunguzi hakutaka tuweke na njia kwa hiyo tumefanya uchunguzi tukatoa matokeo ya uchunguzi kama alivyomba.

Kesi hiyo bado inaendelea kwa usikilizwaji wa mashahidi wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live